Makala

Imeibuka Gen Z ndio wanaofinywa sana na watapeli mitandaoni

Na BENSON MATHEKA August 25th, 2024 1 min read

ONGEZEKO la waathiriwa walio na umri mdogo hasa matineja wanaotapeliwa na wahalifu wa mtandao linaonyesha weledi wa walaghai wa kisasa mtandaoni.

Takwimu mpya zinaonyesha kuwa waathiriwa wengi wa utapeli mtandaoni ni matineja ambao wana ujuzi wa teknolojia na wanaowalenga ni vijana.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ya Hali ya Utapeli wa Mtandao, iliyotolewa na kampuni ya teknolojia ya Social Catfish, kiasi cha pesa zinazopotea kupitia utapeli mtandaoni, na waathiriwa wenye umri wa chini ya miaka 20, kimeongezeka kwa karibu asilimia 2,500 katika kipindi cha miaka mitano, kutoka mwaka 2017 hadi mwaka 2022.

Utafiti  huu unaonyesha mwelekeo ambao matineja na familia zao wanapaswa kuzingatia ili kujinusuru wasitumbukie katika mikono ya matapeli hawa.

Watafiti wanasema kwamba licha ya weledi wao wa teknolojia, matineja na vijana hawajasazwa na wahalifu wa mtandaoni.

Kulingana na utafiti huo, asilimia  24  ya watoto wa umri wa miaka mitatu na minne wanatangamana na mitandao ya kijamii. Hii inaongezeka hadi asilimia   60 kwa watoto wa umri wa miaka minane hadi 11.

Watafiti walisema kuwa ni watoto wachache, chini ya robo ya watoto wote ulimwenguni, wakiwemo matineja walio na weledi wa teknolojia wana uhakika kwamba wanaweza kutofautisha kati ya kilicho halisi na kilicho feki mtandaoni.

Vile vile, ni vigumu kwao kutambua maudhui ya kweli katika mitandao ya kijamii. Kwa hivyo, wazazi wako na jukumu la kuwafahamisha watoto wao kuhusu aina  za ulaghai mtandaoni.

Aina hizo ni pamoja na ushawishi ambapo wahalifu hufungua akaunti bandia za mitandao ya kijamii wakijifanya watu mashuhuri wanazotumia kuwalaghai watu pesa zao  hasa wakilenga  watoto.

Walaghai wanaweza kuandaa shindano la uwongo, kabla ya kumtaka ‘mshindi’ alipe ada au atoe  maelezo ya akaunti ya benki ya mzazi ili kushinda tuzo.