Inasikitisha ni wahudumu 10 pekee wa afya wamefuzu kuajiriwa Uingereza – Kagwe

Inasikitisha ni wahudumu 10 pekee wa afya wamefuzu kuajiriwa Uingereza – Kagwe

Na WANGU KANURI

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesikitikia idadi kubwa ya wahudumu wa afya kufeli kwenye jaribio la mtihani Kiingereza ulionuia kuwapa kazi Uingereza.

Akizungumza katika kufunguliwa kwa mkutano wa kisayansi wa wahudumu wa afya, Waziri Kagwe alidhibitisha kuwa wahudumu kumi pekee wa afya ndio walifuzu katika jaribio la Kiingereza.

Wahudumu hao walikuwa miongoni mwa wengine 300 waliofanya jaribio ambalo lingewasaidia kupata ajira Uingereza.

Mapema mwaka huu, Kenya ilitia saini ya makubaliano ya ajira na Uingereza ili kuwawezesha wahudumu wa afya nchini Kenya kupata kazi nchini Uingereza.

Hii ni baada ya Kenya kuratibu idadi kubwa ya wahudumu wa afya waliofuzu shuleni lakini hawakuwa wamepata ajira.

Hali kadhalika, katika programu hiyo, wahudumu hao wa afya walikuwa waweze kufanya kazi nchini Uingereza kwa miaka kadhaa kabla hawajarejea nchini.

Mshahara wa wahudumu hao wa afya ulikuwa uwe maradufu. Muuguzi kwa mfano alikuwa apate mshahara wa Sh 323,326 kila mwezi akifanya kazi Uingereza ikilinganishwa na mshahara wa Sh 99,620 kila mwezi nchini Kenya.

Hata hivyo, wauguzi hao walikuwa wapate mishahara hiyo ikiwa Kenya ingewatetea wafanyikazi wao kulipwa mishahara sawa na wauguzi wa Uingereza.

Isitoshe, wauguzi wa anaesthesia, wauguzi wa moyo na wauguzi wanaotoa huduma za dharura hawakuwa kati ya wauguzi watakaosafiri kwenda Uingereza.

“Tumepanga mikakati itakayohakikisha kuwa hakutakuwepo na wauguzi wachache nchini baada ya wenzao kuondoka,” akasema Waziri Kagwe.

You can share this post!

Serikali kusaidia waajiri kuboresha maslahi na mazingira ya...

Raila ndiye baba wa ugatuzi, apewe urais 2022 – Junet

T L