Habari Mseto

Inawezekana Samidoh anatamani maisha ya mkewe wa zamani Edday Nderitu?

February 13th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI wa mtindo wa Mugithi Samuel Muchoki Ndirangu almaarufu Samidoh alishangaza mashabiki wake kwa kumfokea shabiki wake wa Facebook aliyemshtumu kuharibu maisha ya ‘aliyekuwa mke wake’, Edday Nderitu.

Wanamtandao hao waliofuata matukio hayo, walionekana kushtuka wengine wakifurahia cheche za majibizano kutoka kwa mwimbaji huyo.

Mwanamuziki huyo tajika, alimtetea mkewe baada ya shabiki mmoja kuchangia kwa madai ya kumharibu maisha ya Eddy Nderitu.

“Umeharibu maisha ya Edday,” alisema Robert Ke.

Ujumbe huo, ulimfanya baba huyo wa watoto watano kumwambia shabiki huyo kuwa maisha ya mkewe Edday Nderitu yako shwari.

“Robert Ke, anaendelea vizuri kuliko baba yako,” alimjibu Samidoh.

Shabiki Fridah Mwaniki alifurahishwa na jinsi mwanamuziki huyo alikabiliana na jumbe za kukera.

“Asante kwa kumtetea mke wako…tunafurahia,” alisema Fridah Mwaniki.

Nancie Muchui alidai kuwa jibu hilo ni dhihirisho kuwa Samidoh anamezea mate maisha ya mkewe.

“Ni rasmi kuwa majibu ya Samidoh yanasema mengi…Anatamani maisha ya Edday,” alisimulia Nancie Muchui.

Katika ujumbe wa awali wenye ucheshi aliopakia Samidoh, ulioandamana na picha akiwa na wanaume wengine sita akiwemo waziri wa michezo Ababu Namwaba, mji wa Boston, Amerika.

“Jamani, mapenzi huwa tu kwa vijana ambao ni matajiri na pia wana msimamo mkali, mimi niliambiwa mapenzi ni sumu na sijiamini. Aki Kanairo wewe,” alipakia Samidoh.

Chapisho hilo, lilisababisha majibizano wengi wakihisi anamtetea mkewe Edday Nderitu ambaye anaishi Amerika pamoja na wanawe watatu.

Mwanamuziki huyo yupo Amerika kuwatembelea wanawe watatu, wakati wa ziara yake fupi nchini humo.