Indonesia yaharamisha ngono nje ya ndoa

Indonesia yaharamisha ngono nje ya ndoa

NA MASHIRIKA

JAKARTA, Indonesia

BUNGE la Indonesia limeifanyia marekebisho sheria ya uhalifu nchini humo kwa kuharamisha ngono nje ya ndoa.

Bunge hilo pia limepitisha sheria inayodhibiti uhuru wa kujieleza katika hatua inayoonekana kuhujumu haki katika taifa hilo linaloheshimika kwa kukumbatia utawala wa kidemokrasia.

Huku ikiungwa mkono na vyama vyote vya kisiasa, sheria hiyo dhalimu imeshtua sio tu wanaharakati wa kutetea haki nchini Indonesia lakini sekta ya utalii, ambayo hutegemea wageni ambao hutembelea visiwa vyake.

Hii ni kwa sababu watalii wanaozuru Indonesia, wengi wao wakiwa kutoka Australia pia wataathirika na sheria hiyo ikizingatiwa kuwa wao ndio huzuru nchini humo kwa wingi.

“Kile tunachoshuhudia ni pigo katika maendeleo yaliyofikiwa na Indonesia katika kulinda haki za kimsingi za kibidamu ndani ya miongo miwili,” akasema Usman Hamid, ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki, Amnesty International, tawi la Indonesia.

“Kupiga marufuku ngono nje ya ndoa na sawa na kuhujumu haki ya usiri ya watu inayolindwa chini ya sheria ya kimataifa,” Hamid akasema.

“Mahusiano ya kimapenzi ya hiari hayapaswi kuchukuliwa kama kosa la uhalifu au ukiukaji wa maadili,” akaongeza.

Balozi wa Amerika nchini Indonesia, Sung Kim, alionya kuwa sheria hiyo inahujumu maslahi ya kimataifa ya Indonesia.

“Kuharamisha maamuzi ya kibinafsi ya watu kunaweza kuogofya kampuni ambazo zingependa kuwekeza nchini Indonesia,” akasema.

Tafsiri: Na CHARLES  WASONGA

You can share this post!

Kaunti ya Kilifi yaweka mikakati ya kuwashughulikia...

Murkomen ataja hatua zinazolenga kupunguza vifo Thika...

T L