Michezo

INEOS 1:59 Challenge: Dunia kusimama Eliud Kipchoge akiendea rekodi Marathon

October 9th, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ELIUD Kipchoge anatarajiwa kuwa kivutio cha mabilioni ya wapenzi wa riadha watakaojitokeza katika barabara za jiji la Vienna, Austria na kumfuatilia kwa namna zozote atakapotifua kivumbi wikendi hii.

Bingwa huyu wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, atapania kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili.

Ni tukio la kihistoria linalotazamiwa kuibua msisimko wa aina yake duniani kote.

Ili kufanikisha hatua za mwisho za maandalizi ya Kipchoge, bilionea mmiliki wa kampuni ya INEOS kutoka Uingereza, Sir Jim Ratcliffe aligharimia safari ya ndege ya kibinafsi aina ya Gulfstream yenye thamani ya Sh2.4 bilioni iliyomjia mwanariadha huyu humu nchini mnamo Jumatatu.

 

Mshikilizi wa Rekodi ya Dunia ya mbio za Marathon, Eliud Kipchoge (kati) alipoabiri ndege kuelekea Prater, Vienna, Austria. Picha/ Jared Nyataya

Mbali na kocha Patrick Sang na daktari Peter Nduhiu, wengine waliosafiri pamoja na Kipchoge katika ndege hiyo ya haiba kubwa ni Augustine Choge na Gideon Kipketer watakaokuwa sehemu ya watimkaji saba wa kumtia motisha ya kuongoza kasi yake.

Kipchoge, 34, alivunja rekodi ya dunia mwaka 2018 kwa kukamilisha kivumbi cha Marathon kwa muda wa saa 2:01:39 nchini Ujerumani.

Hata hivyo, nusura rekodi yake hiyo ifutwe na Mwethiopia Keninisa Bekele, 37, aliyekamilisha mbio zizo hizo za Berlin Marathon kwa muda wa saa 2:01:41 nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki iliyopita.

Atashuka ulingoni jijini Vienna kuanzia saa tatu asubuhi kwa minajili ya kipute cha INEOS 1:59 Challenge.

Hadi alipoondoka humu nchini, Kipchoge alikuwa akijifua katika miji ya Kaptagat, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet na Eldoret, Uasin Gishu.

“Kipchoge atavunja nyingi za rekodi zake mwenyewe,” akasema Rais wa FKF, Nick Mwendwa.