Habari

INEOS 1:59 Challenge: Eliud Kipchoge afaulu kukamilisha mbio za Marathon chini ya muda wa saa mbili

October 12th, 2019 1 min read

Na ELIAS MAKORI akiwa VIENNA, AUSTRIA

MKENYA Eliud Kipchoge ameweka historia Jumamosi kwa kuwa binadamu wa kwanza kukimbia mbio za Marathon chini ya muda uliozoeleka wa saa mbili baada ya kutumia muda wa saa 1:59:40 katika jaribio lenye umaarufu la INEOS 1:59 Challenge katika Prater Park jijini Vienna, Austria.

Kipchoge ambaye alisaidiwa na wadhibiti kasi 41, anaingia katika kitabu cha historia cha Guinness Book of World Records kwa kukamilisha mbio chini ya muda wa saa mbili ingawa rekodi yake haitatambuliwa na chombo cha riadha duniani, IAAF, kama rekodi mpya ya mbio hizo za Marathon.

Mwaka 2017 katika jaribio lake la kwanza, mwanariadha huyo alikosea kwa sababu alikuwa nyuma ya muda aliolenga kwa sekunde 26 wakati wa “Breaking2” mjini Monza, Italia ambapo aliweka muda wa saa 2:00:25.