Michezo

INEOS 1:59 Challenge: Eliud Kipchoge ahitaji spidi ya duma

October 10th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge amesema ameridhishwa na hali ya hewa na ubora wa barabara itakayotumiwa kwa marathon za INEOS1:59 Challenge mwishoni mwa wiki hii jijini Vienna, Austria.

Bingwa huyu wa Olimpiki mwenye umri wa miaka 34 atapania kuweka historia ya kuwa binadamu wa kwanza duniani kukamilisha marathon ya kilomita 42 kwa muda wa chini ya saa mbili yaani dakika 119 au sekunde 7,140.

Ili kuiweka rekodi hii mpya anayoiendea nchini Austria, itamlazimu Kipchoge kukimbia kwa kasi itakayomwezesha kukamilisha kila hatua ya mita 5.8 kwa kipindi cha sekunde moja.

Kipchoge aliwasili Vienna mnamo Jumanne na kuanza maandalizi kwa kivumbi hicho kitakachoandaliwa mnamo Jumamosi hii kuanzia saa mbili asubuhi.

Atakuwa akitiwa motisha na wanariadha wengine 41 watakaojitokeza katika hatua mbalimbali ili kuongoza kasi yake.

“Nimeridhishwa na hali ya hewa na namna kila kitu kinavyozidi kuwekwa sawa. Nimezungushwa kwenye barabara nzima nitakayoikimbilia na nimejionea kwamba iko sawa,” akasema Kipchoge katika mahojiano yake ya Jumatano na shirika la BBC.

Kipchoge aliondoka humu nchini mnamo Jumatatu kwa hisani ya bilionea mzawa wa Uingereza na mmiliki wa kampuni ya INEOS, Sir Jim Ratcliffe.

Alisafirishwa hadi Vienna kwa ndege ya kibinafsi aina ya Gulfstream G280 yenye thamani ya Sh2.4 bilioni iliyomjia katika kambi yake ya mazoezi mjini Eldoret, Uasin Gishu.

Mbali na kocha Patrick Sang na daktari Peter Nduhiu, wengine waliosafiri na Kipchoge katika ndege hiyo ya haiba kubwa iliyomjia mwanzoni mwa wiki hii ni Augustine Choge na Gideon Kipketer watakaokuwa sehemu ya watimkaji watakaokimbia naye.

Ndege hiyo yenye injini mbili za Honeywell HTFT250G zinazoifanya kuwa miongoni mwa ndege zenye kasi zaidi ulimwenguni, ilikuwa ikiendeshwa na marubani wawili kutoka Uingereza.

Kipchoge anatarajiwa kuwa kivutio cha mabilioni ya wapenzi wa riadha watakaojaa kwenye vichochoro na barabara za jiji la Vienna kumtilia shime, na hata kumfuatilia kwa namna zozote ulimwenguni wakati wa kivumbi hicho.

Jaribio hili la Kipchoge tayari limeanza kuibua msisimko wa aina yake huku mwanariadha wa kike mzawa wa Uhispania, Paula Cobo, akitua humu nchini yapata majuma mawili yaliyopita kumtakia Kipchoge kila la heri na pia kuanika ukubwa wa kiwango cha jinsi anavyomstahi mfalme huyu wa dunia kwa ‘pendo halisi’.

“Ninampenda Kipchoge kwa moyo wa dhati. Ninamtakia fanaka na heri njema katika kibarua chake kijacho. Itakuwa tija na fahari yangu kushuhudia akivunja rekodi yake mwenyewe katika mbio za marathon,” akasema Cobo aliyeandamana na baadhi ya marafiki zake.

Isitoshe, Safaricom imebadilisha nembo yake ya M-Pesa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 12 kwa heshima ya Kipchoge ambaye kwa sasa ni balozi mpya wa kampuni hiyo ya huduma za mawasiliano.

Kwa mujibu wa Michael Joseph, ambaye ni kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, nembo hiyo kwa sasa itakuwa ‘Eliud 1:59’ na itadumu kwa kipindi cha siku saba zijazo. Safaricom pia itatoa huduma za bure kwa wateja wake wote watakaoazimia kumfuatilia Kipchoge kupitia YouTube siku ya kuandaliwa kwa kivumbi cha INEOS1:19 Challenge.

“Tulikuwa wa kwanza kabisa kuwapa walimwengu huduma ya kutuma na kutoa pesa kupitia simu mnamo 2007. Kenya pia itakuwa ya kwanza kutoa mwanariadha atakayelenga kukamilisha mbio za mita 42,000 (42km) chini ya muda wa saa mbili,” akasema Joseph.

Kipchoge alivunja rekodi ya dunia mwaka jana kwa kukamilisha kivumbi cha Berlin Marathon kwa muda wa saa 2:01:39 nchini Ujerumani.

Hata hivyo, nusura rekodi yake hiyo ifutiliwe mbali na Mwethiopia Keninisa Bekele, 37, aliyekamilisha mbio za Berlin Marathon kwa muda wa saa 2:01:41 nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki iliyopita.

Hadi alipoondoka humu nchini, Kipchoge alikuwa akijifua mjini Eldoret na katika eneo la Kaptagat, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet ambapo alidhihirisha kuwa anaweza kuvunja rekodi hiyo.

Mbio za mita 5,000

Akiwa na umri wa miaka 18 pekee, Kipchoge alitawazwa mfalme wa mbio za mita 5,000 katika Riadha za Dunia mnamo 2003 nchini Ufaransa.

Ufanisi huo ulifuatwa na nishani ya shaba katika Olimpiki za 2004 kabla ya kuinyakulia Kenya medali nyingine ya shaba katika mbio za IAAF mnamo 2006.

Akiwa mwanafainali mara tano wa mbio za mita 5,000 duniani, alinyakua nishani za shaba katika Riadha za Dunia mnamo 2007, Olimpiki za 2008 na Jumuiya ya Madola mnamo 2010.

Mnamo 2012, alihamia katika mbio za masafa marefu na kuandikisha muda wa dakika 59:25 katika Nusu Marathon.

Muda huo ndio wa pili kwa ubora zaidi katika historia ya mbio hizo.

Hambourg Marathon ilikuwa ya kwanza kabisa kwa Kipchoge kushiriki mnamo 2013. Ushindi wa kwanza katika mbio hizo ulimjia mnamo 2014 katika Chicago Marathon. Hadi alipoweka rekodi mpya katika mbio za marathon, ndiye aliyekuwa mfalme mara tatu wa London Marathon na Berlin Marathon.

Akichukuliwa kuwa mkimbiaji bora zaidi katika historia ya marathon, anajivunia ushindi katika marathon 11 kati ya 12 ambazo amezishiriki kufikia sasa.

Mabilionea wengi wameahidi kumtuza mabilioni ya pesa iwapo atakimbia mbio hizo chini ya saa mbili. Mnamo Jumanne, bilionea wa Uingereza, Jim Ratcliffe, alituma ndege yake ya kibinafsi imchukue Kipchoge kutoka mjini Eldoret hadi Austria ambapo mbio hizo zitafanyika Jumamosi.

Ratcliffe pia ndiye mmiliki wa kampuni kwasi ya kutengeneza kemikali ya Inspec Ethylene Oxide Specialities (INEOS) ambayo inadhamini mbio hizo.