Michezo

Ingosi na Akida wa Harambee Starlets waanika maazimio yao soka ya klabu ng'ambo

July 30th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO mkabaji wa Harambee Starlets, Ruth Ingosi, amefichua mipango yake ya msimu ujao katika kikosi cha FC Lakatamia nchini Cyprus.

Ingosi aliingia katika sajili rasmi ya Lakatamia mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kuagana rasmi na klabu ya Eldoret Falcons. Alikosa fursa ya kuoanisha vilivyo mtindo wake mchezo wake na wa wanasoka wenzake kikosini baada ya kampeni za msimu kuvurugwa na janga la corona.

Hadi Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Cyprus ilipotamatishwa ghafla mnamo Machi 2020, zaidi ya robo tatu za mechi za muhula huu zilikuwa zimesakatwa. Ingosi aliwezeshwa kutandaza michuano minne pekee iliyomshuhudia akifunga mabao mawili na kusaidia waajiri wake hao kukamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la vikosi 12.

Wanasoka wa FC Lakatamia wanatarajiwa kurejea kambini wiki ijayo kwa minajili ya kujifua kwa msimu mpya utakaoanza Septemba. Ingosi ameshikilia kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwatambisha waajiri wake katika msimu wa 2020-21 kwa matumaini ya kukamilisha kampeni miongoni mwa vikosi viwili vya kwanza na kufuzu kwa soka ya bara Ulaya.

Apolon Ladies ambao ni malkia wa Ligi Kuu ya Cyprus, watashiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa upande wa akina dada msimu ujao.

Katika malengo binafsi, Ingosi anapania kufunga zaidi ya mabao 10 na kuwa miongoni mwa wawaniaji halisi wa taji la wafungaji bora ligini.

“Natazamia kuwa na maandalizi maridhawa kwa minajili ya msimu mpya. Sikuwa na muda wa kutosha kuzoea mitindo ya kucheza kwa wanasoka wenzangu kikosini msimu uliopita. Sasa tutaanza upya pamoja na sitakuwa na sababu ya kutofikia malengo yangu,” akasema Ingosi, 22.

Ingosi alikuwa sehemu ya kikosi cha Starlets kilichoongozwa na kocha David Ouma kutia kapuni ubingwa wa Cecafa Challenge Trophy nchini Tanzania mnamo Disemba 2019. Alikuwa pia tegemeo katika michuano ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo.

Kwingineko, mvamizi Esse Akida wa Starlets atanogesha soka ya Europa League msimu ujao akivalia jezi za kikosi cha Besiktas nchini Uturuki. Hii ni baada ya kampeni za Ligi Kuu msimu huu kutamatishwa Besiktas wakishikilia nafasi ya pili kwa alama 42, moja nyuma ya ALG Spor.

Besiktas walimsajili Akida, 27, kutoka klabu ya Hapoel Ramat HaSharon FC ya Israel mnamo Februari 2020.

Hadi Ligi Kuu ya Uturuki ilipohitimishwa, Akida alikuwa amewajibishwa na Besiktas mara mbili katika kipute hicho kilichokuwa kimefikia raundi ya mechi 15.

Kabla ya kuyoyomea Israel kuchezea FC Ramat, Akisa alikuwa mchezaji wa klabu za Spedag na Thika Queens zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KWPL).

Alipokea malezi yake ya awali kabisa kwenye ulingo wa soka katika klabu ya Moving The Goalposts (MTG) kabla ya kuhemewa na Spedag kisha Thika Queens.

Baada ya kujipatia umaarufu akivalia jezi za Starlets katika fainali za Kombe la Afrika (AWCON) nchini Cameroon mnamo 2016, Akida alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Starlets kilichotegemewa na kocha David Ouma kwenye soka ya COTIF jijini Valencia, Uhispania mwaka uo huo. Aliibuka mchezaji bora zaidi (MVP) katika kivumbi hicho.

Akida alivalia jezi za Starlets kwa mara ya mwisho mnamo 2018 katika fainali za Cecafa zilizoandaliwa jijini Kigali, Rwanda.