Michezo

Ingwe kutegemea huduma za Rupia kwa miaka 4

June 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

AFC Leopards wamesema kwamba mipango ya kumdumisha mvamizi Elvis Rupia kambini mwao kwa kipindi cha miezi 48 zaidi ipo katika hatua za mwishomwisho.

Mkataba kati ya fowadi huyo na Leopards ulitamatika rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita na Mwenyekiti Dan Shikanda amesema kwamba ofisi yake inajitahidi kumshawishi Rupia kutia saini mkataba mpya wa muda mrefu.

“Tumepiga hatua kubwa katika mazungumzo ya kumsadikisha kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Leopards baada ya kocha Anthony Kimani na maafisa wenzake katika benchi ya kiufundi kupendekeza hivyo,” akasema Shikanda.

Rupia alijiunga na Leopards mnamo Januari 2020 baada ya kuagana na Wazito FC. Kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Wazito, Rupia aliwahi pia kuchezea Nzoia Sugar na Power Dynamos ya Ligi Kuu ya Zambia.

Kanuni mpya zinazozuia watu kuingia na kutoka jijini Nairobi ni jambo ambalo Rupia amesema kwamba limemzuia kukamilisha hatua za mwisho za kurasimisha mkataba wake mpya na Leopards licha ya kupokea ofa kutoka kwa baadhi ya klabu maarufu za KPL na nyinginezo kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki.

“Benchi ya kiufundi imefichua azma ya kuendelea kujivunia huduma zangu kambini mwa Leopards. Baada ya masharti kuhusu usafiri wa kuingia na kutoka ndani ya Nairobi kulegezwa, nitatia wino kwenye kandarasi mpya ya Leopards ambao wamedokeza kwamba haitapungua miaka minne,” akasema.

Kwa upande wake, Shikanda amesisitiza kwamba hawatamkwamilia Rupia iwapo atashawishika kukubali ofa za kikosi kingine kinginecho kitakachokuwa radhi kumdumisha vyema kimshahara na kumpa jukwaa mwafaka zaidi la kuyafikia mengi ya maazimio yake kitaaluma.

“Sera zetu kuhusu usajili wa wachezaji zinaeleweka vyema. Hatuwezi kuzuia wala kumhangaisha mchezaji yeyote aliyepata ofa bora zaidi kuliko ile tunayompokeza. Milango yetu ipo wazi siku zote kwa wanasoka wetu wanaopania kujikuza na kujiendeleza zaidi kitaaluma katika mataifa mengine,” akatanguliza Shikanda.

“Iwapo Rupia amepania kutafuta hifadhi mpya kwingineko, basi itatulazimu kumwachilia na kutafuta mvamizi mwingine. Tungependa sana atie saini mkataba mpya mtandaoni ila tunataka afanye hivyo kadamnasi na tukio hilo kuangaziwa na vyombo vya habari,” akaongeza kinara huyo.