Michezo

Ingwe mawindoni kusafisha rekodi yake duni dhidi ya Stima

March 22nd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards inatarajiwa Jumamosi kuwa na kibarua kigumu dhidi ya Western Stima itakapoalika klabu hii kutoka kaunti ya Kisumu ambapo Ingwe watakuwa wenyeji katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.

Leopards, ambayo itaruka kutoka nafasi ya 17 hadi nambari 13 ikilemea Stima, imekuwa ndani ya maeneo hatari ya kutemwa ama alama chache nje ya mduara huu kwa kipindi kikubwa msimu huu. Haina ushindi dhidi ya Stima katika mechi nne zilizopita.

Mabingwa mara 13 Leopards walishinda wanaumeme wa Stima mara ya mwisho mwaka 2015 walipowazima 1-0 katika mechi ya mkondo wa pili. Ingwe ilipoteza nyumbani na ugenini dhidi ya Stima msimu 2016 na kukubali wanaumeme hao kutoa alama nne dhidi yao mwaka 2017.

Rekodi hii inaiweka Leopards katika nafasi mbaya kabla ya mchuano huu ambao inahitaji ushindi ili kujiondoa katika mduara hatari wa kutemwa.

Vijana wa Casa Mbungo waliingia katika mduara hatari katikati mwa juma baada ya Zoo kuambulia alama moja muhimu dhidi ya Nzoia Sugar na kuruka juu nafasi moja hadi nambari 16.

Zoo wako mbele ya Ingwe kwa tofauti ya magoli. Klabu hizi mbili zimezoa alama 16 kutokana na mechi 18 na 17, mtawalia.

Leopards itapata motisha ya kutafuta ushindi kutokana na kwamba Stima ni mojawapo ya timu zinazofanya vibaya sana wakati huu.

Stima haina ushindi katika mechi tano zilizopita baada ya kukubali sare dhidi ya Gor Mahia (mabingwa watetezi), Vihiga United na Mathare United na kulimwa bila kufunga bao dhidi ya SoNy Sugar na Chemelil Sugar.

Ingwe iliajiri mchezaji wake wa zamani Anthony Kimani kuwa msaidizi wa Mbungo. Baada ya kuteuliwa kwake Machi 19, mashabiki walimtaka asaidie kurekebisha ngome ya Leopards inayovuja.

Baadhi yao hawakuridhika na kuteuliwa kwake kwa hivyo mechi hii yake ya kwanza ni mtihani kwake.

Itawapa wakosoaji wake sababu ya kuendelea kumpapura Ingwe isipopata matokeo mazuri dhidi ya Stima.

Mechi nyingine itakayosakatwa Jumamosi itakutanisha Chemelil Sugar na Bandari mjini Chemelil.

Wakati moja Bandari ilionekana kuwa mgombeaji halisi wa taji, Hata hivyo, imefifia. Imeambulia alama moja katika mechi tatu zilizopita.

Sofapaka inaongoza kwa alama 33 kutokana na mechi 18 ikifuatiwa alama moja nyuma na Gor, ambayo haijasakata mechi mbili.

Bandari ni ya tatu kwa alama 32 baada ya kucheza mechi 17.

Baada ya kupoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya SoNy Sugar na Ulinzi Stars, Bandari itakuwa na presha ya kupata ushindi angaa ifufue matumaini ya kusalia katika mbio za kuwania taji.

Ratiba:

Machi 23

AFC Leopards na Western Stima (Machakos, 3.00pm),

Chemelil Sugar na Bandari (Chemelil, 3.00pm)

Machi 24

Posta Rangers na KCB (Machakos)

Machi 26

Tusker na Kariobangi Sharks (Ruaraka, 3.00pm)