Michezo

Ingwe na Sharks nguvu sawa

April 24th, 2019 1 min read

NGUVU mpya George Abege Jumatano Aprili 24 alifunga bao katika dakika za lala salama na kuhakikisha timu yake ya Kariobangi Sharks inalazimisha sare ya 1-1 dhidi ya AFC Leopards kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Kenya(KPL) iliyosakatwa ugani MISC Kasarani.

AFC Leopards ambao ni mabingwa mara 13 wa KPL walianza mechi hiyo kwa matao ya juu na hata kuchukua uongozi kunako kipindi cha kwanza kupitia bao la Whyvonne Isuza, sekunde 30 tu baada ya mechi kuanza.

Sajili mpya Paul Were alimmegea Isuza, ambaye anaongoza orodha ya wafungaji wa Ingwe msimu huu wa 2018/19 kwa mabao sita pasi safi na kumwezesha kufunga bao hilo. 

Hata hivyo, wachezaji wa timu zote mbili walionyesha utovu wa nidhamu uwanjani na mwaamuzi wa mechi akalazimika kuingilia kati kila mara ili kuwatenganisha na kuwapa onyo.

Ingawa hivyo, Kariobangi Sharks walipata pigo katika dakika 62 pale Ian Taifa alipolishwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya mlinzi wa Ingwe Isaac Kipyegon baada ya refa kumwonya mara kadhaa. Hatua hiyo ilizima kabisa mashambulizi ya awali yaliyolenga lango la Leopards yaliyoongozwa na mshambulizi matata wa Sharks, Patilah Omoto.

Vijana wa Kocha Casa Mbung’o hata hivyo walikosa kutumia vyema nafasi kadhaa walizopata huku mlinzi Yusuf Mainge akikosa kufunga bao la wazi baada ya kumwacha hoi mnyakaji wa wapinzani Jeff Oyemba.

Hatua ya mkufunzi wa Sharks William Muluya kumwondoa Mganda Sydney Lokale na kumuingiza Abege zilizaa matunda katika muda wa ziada pale aliporuka juu ya walinzi wa Ingwe na kufunga mpira wa ikabu iliyokuwa imechanjwa kiustadi na kiungo Duke Abuya katika muda wa ziada.

Matokeo haya yanawaacha Leopards katika nafasi ya 10 kwa alama 30, alama mbili nyuma ya Sharks inayoshikilia nafasi ya tisa ingawa Ingwe bado haijawajibikia mechi moja ikilinganishwa na wapinzani wao.