Michezo

Ingwe wasajili mnyakaji wa UG Ochan

July 16th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) AFC Leopards wamemsajili aliyekuwa mnyakaji wa timu ya taifa ya Uganda Benjamin Ochan kwa kandarasi ya mwaka moja.

Mnyakaji huyo wa zamani wa Uganda Cranes amekuwa akidakia Kabwe Warriors ya Zambia lakini alitamatisha kandarasi yake ghafla siku chache zilizopita katika kile kinachodaiwa kukosa kuelewana na wakuu wa klabu hiyo kuhusu mshahara wake.

Kulingana na ajenti wake, Ochan alipata ofa kadhaa kutoka kwa baadhi ya klabu mahiri za soka barani Afrika ila akachagua Ingwe kutokana na historia yake pevu kwenye soka nchini.

“Benjamin Ochan atakuwa akichezea AFC Leopards msimu ujao. Tumekuwa na ofa nyingi mezani lakini tumeamua kukumbatia ofa ya Ingwe,” akasema ajenti wake huku akifichua veterani huyo atajiunga na wachezaji wenzake wakati wa kambi ya kujifua jijini Kisumu wiki hii.

AFC Leopards imekuwa ikitafuta nyani wa kurithi nafasi ya Eric Ndayishimiye aliyejiunga na AS Kigali ya Rwanda.

Ochan alianza taaluma yake ya soka katika akademia ya vijana ya Entebbe. Amewahi kuzisakatia Aahus Gymanastikforening ya Denmark, KCCA ya Uganda, Bloemfontein Celtic ya Afrika Kusini kabla ya kujiunga na Kabwe Warriors.