Ingwe washikwa na wasiwasi kuhusu udhamini wa Betika

Ingwe washikwa na wasiwasi kuhusu udhamini wa Betika

NA JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards imeingiwa na wasiwasi kuwa huenda ikapoteza udhamini wa Betika kutokana na kutofahamika ni lini msimu mpya wa 2022/23 utaanza.

Mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda alisema Betika ambayo ilitia saini udhamini AFC Leopards kwa kima cha Sh195 milioni miezi michache iliyopita, huenda ikapata ugumu wa kuendelea kuwafadhili ilhali hakuna soka inayoendelea.

Udhamini wa Betika kwa Ingwe unastahili kuendelea kwa muda wa miaka mitatu na Shikanda anadai kuwa hata timu nyingine pia zipo katika hatarini kupoteza ufadhili wao kama hakuna ligi.

Msimu mpya bado haujaanza huku wengi wakisubiri Waziri Mpya wa Michezo aliyeteuliwa na Rais William Ruto, Ababu Namwamba apigwe msasa na kamati ya bunge na aapishwe. Wanatarajia Namwamba atatoa mwelekeo kuhusu marufuku ambayo Kenya inatumikia ya Fifa.

Timu zinazoshiriki Ligi Kuu (KPL) chini ya vuguvugu lao nazo zimeapa kuwa hazitashiriki mechi zozote za msimu mpya hadi marufuku hiyo iondolewe kwa sababu imeathiri wachezaji na wanaotegemea soka.

“Naomba kuwa utata huu unaozingira soka utatuliwe mara moja kwa sababu unaweka udhamini wetu hatarini. Tuna mdhamini ambaye amewekeza zaidi katika timu yetu ila iwapo hakutakuwa na soka inayochezwa basi tutakuwa hatarini,” akasema Shikanda.

“Bado hatujapokea mawasiliano yoyote kuhusu ni lini msimu mpya utaanza. Bado tunasubiri tufahamu ni lini ila tuna matumaini itakuwa hivi karibuni,” akaongeza Shikanda.

Mwanzoni msimu mpya uliratibiwa ungeanza Septemba 10 ila ukaahirishwa hadi Septemba 24. Kamati ya Mpito ambayo imekuwa ikisimamia soka ilitangaza kuwa ilistahili kuanza mnamo Oktoba 1 lakini ikaahirisha kwa mara nyingine bila kutangaza tarehe mpya.

“Tunataka utata huu wa Fifa upate suluhu ili mpira urejee kama zamani nao wale ambao wananufaika kutokana na mpira wasipoteze ajira. Kwetu ujio wa Betika ulikuwa nafuu kwetu na nina hakika nao watapata thamani ya ufadhili wao,” akaongeza Shikanda.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Karani anayekuza mboga za kienyeji

Malkia wa vita vya masumbwi Achieng’ kulimana na Melissa...

T L