Michezo

Ingwe wawinda Mnigeria anayesakata Uganda

June 25th, 2018 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Baada ya juhudi zao za kumpata straika Elvis Rupia wa Nzoia United kuambulia patupu, huenda AFC Leopards ikamsaini raia wa Nigeria anayesakata nchini from Rwanda.

Ingwe ambayo tayari imewaleta wachezaji watatu klabuni, wanakaribia kumpata Alex Orotomal kutoka klabu ya Sunrise FC.

Nyota huyo anashikilia nafasi ya nne katika orodha ya ufungaji mabao ligini nchini Rwanda, akijivunia mabao 10, matatu tu nyuma ya mzalendo, Ndarusanze Claude.

“Alex anatarajiwa kufika Nairobi wiki hii kufanya mashauriano na wakuu wa Leopards kabla ya mkataba kuandikishwa,” afisa ambaye hakutaka kujulikana alisema.

Mbali na Alex, Leopards wanafanya mazungmzo na Mganda, Abraham Ndungwa kuiongezea nguvu safu yao ya ulinzi.

Mabingwa hao wa GOtv ambao kesho Jumatano watakuwa ugenini kucheza na Zoo wamesema mechi hiyo itakayochezewa Kericho Green Stadium itaanza saa tisa.

Mashabiki watalipa Sh200 kuingia uwanjani humo.

Timu hizo zilitoka sare 2-2 zilipokutana kwa mara ya mwisho uwanjani Kenyatta Stadium, Machakos.

Katika mechi zao za majui, Zoo ilitoka sare 1-1 na  SoNy Sugar wakati Ingwe ikiibwaga Chemelil 2-0 mjini Machakos. Jumapili, vijana hao wa kocha Zapata Rodolfo waliwanyuka Rainforest 4-0 na kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya michuano ya Shield Cup.