Michezo

Ingwe yang’aria Sofapaka tena mechi ya ligi KPL

February 22nd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards ilionjesha Sofapaka makali yake baada ya kuichabanga 2-1 katika mechi ya kusisimua ya Ligi Kuu (KPL) uwanjani Mumias Complex, Jumamosi.

Leopards almaarufu Ingwe, ambayo pia ilizima Batoto ba Mungu 2-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza Oktoba 2019 ilipata mabao yake kupitia kwa mshambuliaji Elvis Rupia dakika ya 51 na 78. Sofapaka ilijiliwaza na bao la Jedinak Ameyaw kabla tu ya kipenga cha mwisho kulia.

Vijana wa Anthony Kimani, ambao walikuwa wamepoteza 1-0 dhidi ya Tusker katika mechi iliyopita, wanafunga mduara wa tano-bora kwa alama 37 baada ya kuruka juu nafasi moja.

Sofapaka, ambao walikuwa wamechapa mabingwa watetezi Gor Mahia 3-1 katika mechi iliyopita, wako nafasi ya nane kwa alama 30.

Wanabenki KCB walifuta vichapo vya mechi mfululizo dhidi ya Kariobangi Sharks na Bandari, kwa kuliza Posta Rangers 3-1 uwanjani Kenyatta mjini Machakos. Enock Agwanda alitikisa nyavu mara mbili naye Michael Mutinda akachangia bao moja.

Katika mechi iliyofungua siku hapo Jumamosi, Bandari ilitumia uwanja wake wa nyumbani wa Mbaraki kupepeta Mathare United 3-1.

Abdallah Hassan, William Wadri na Yema Mwana walifunga mabao ya Bandari, ambayo sasa imezoa ushindi mbili mfululizo baada ya kuchabanga KCB 2-1.

John Mwangi alifungia Mathare bao la kujiliwaza.

Uwanjani Moi mjini Kisumu, Western Stima na Kariobangi Sharks waliumiza nyasi bure katika sare ya 0-0.