Michezo

Ingwe yang'olewa kucha na Wazito FC

August 30th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

AFC Leopards ilitupa uongozi wa bao moja na kushangazwa 2-1 na Wazito katika mechi za raundi ya 29 za Ligi Kuu iliyoshuhudia Kariobangi Sharks na Ulinzi Stars zikivuna ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya Thika United na Nakumatt, mtawalia, Jumatano.

Mashabiki wa Leopards walikuwa na matumaini makubwa timu yao itafuta kichapo cha mabao 2-0 ilichopokea kutoka kwa mahasimu wa tangu jadi Gor Mahia kwa kupepeta limbukeni Wazito. Matumaini yaliongezeka ilipochukua uongozi kupitia mshambuliaji wa Nigeria, Alex Orotomal dakika ya 23 na kuenda mapumzikoni na uongozi huo mwembamba.

Hata hivyo, raha ya kuongoza dakika 45 za kwanza iligeuka kuwa kiraha pale Wazito ilisawazisha kupitia Derrick Onyango sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza kabla ya David Oswe kugonga msumari wa mwisho dakika ya 90.

Ingawa Wazito ilisalia wachezaji 10 uwanjani dakika ya tatu ya majeruhi baada ya Jackson Saleh kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, Leopards haikuweza kulazimisha sare angaa kupata alama.

Leopards inasalia katika nafasi ya tatu kwa alama 48, nyuma ya viongozi Gor Mahia (71) na nambari mbili Bandari (51). Wazito ni ya pili kutoka mwisho kwa alama 27. Thika United inavuta mkia kwa alama 20 baada ya kupoteza mechi ya sita mfululizo. Thika imeambulia alama mbili kutoka mechi zake 11 zilizopita.

Matokeo (Agosti 29, 2018):

Kariobangi Sharks 3-0 Thika United (Machakos), Posta Rangers 0-1 Sofapaka (Camp Toyoyo), Tusker 2-0 Chemelil Sugar (Ruaraka), Ulinzi Stars 3-0 Nakumatt (Nakuru), Wazito 2-1 AFC Leopards (Machakos).