Michezo

Ingwe yaponea kichapo

April 8th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards imetoka nyuma mabao mawili na kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Nzoia Sugar kwenye Ligi Kuu mjini Mumias, Jumapili.

Nazo Mathare United, Kakamega Homeboyz na Thika United zimevuna alama tatu muhimu kila mmoja baada ya kuzima wapinzani wao.

Nzoia iliongoza 2-0 kabla ya Brian Marita kurejesha goli moja dakika ya 42 naye Robinson Kamura akahakikishia Ingwe alama aliposawazisha dakika tatu baada ya kipindi cha pili kuanza.

Mathare, ambayo ilikuwa imepoteza mechi tatu mfululizo Tusker, ilimaliza mikosi hiyo kwa kubwaga wanamvinyo hao 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani wa Ruaraka, Nairobi.

Mavamizi John Mwangi alifungia Mathare bao hilo la pekee katika dakika ya 44 kupitia kichwa chake. Ushindi huu ni wa nne mfululizo wa mabingwa wa mwaka 2008 Mathare msimu huu.

Homeboyz ilifurahisha mashabiki wake wa nyumbani baada ya kuongeza masaibu ya Nakumatt kwa kuipiga 2-0 uwanjani Bukhungu, Kakamega. Nakumatt, ambayo haina ushindi katika mechi sita sasa, ilizamishwa na mabao ya Moses Mudavadi na Estone Esiye.

Thika, ambayo haikuwa imeshinda mechi tangu msimu uanze Februari 3, hatimaye inatabasamu baada ya kuduwaza mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka 2-1. Ni ushindi wa kwanza wa Thika dhidi ya Sofapaka katika mechi saba.

Matokeo (Aprili 8, 2018): SoNy Sugar 2-2 Kariobangi Sharks, Vihiga United 1-1 Chemelil Sugar, Bandari 1-1 Ulinzi Stars, Kakamega Homeboyz 2-0 Nakumatt, Mathare United 1-0 Tusker, Thika United 2-1 Sofapaka, Zoo 1-0 Posta Rangers.