Michezo

Ingwe yararua Zoo nayo Ulinzi yazima Rangers

January 6th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa zamani AFC Leopards na Ulinzi Stars walifanikiwa kulipiza kisasi dhidi ya Zoo na Posta Rangers kwenye Ligi Kuu mtawalia, Jumapili.

Uwanjani Bukhungu mjini Kakamega, wenyeji Leopards almaarufu Ingwe waliuma Zoo 3-1 baada ya kuongoza 2-0 wakati wa mapumziko kupitia mabao ya Bonface Mukhekhe na John Makwata.

Mukhekhe alifuma wavuni bao safi kupitia kichwa chake baada ya kupokea kona kutoka kwa Austin Odhiambo dakika ya 13.

Makwata aliimarisha uongozi huo kupitia ikabu dakika ya 42 baada ya Collins Shivachi kuchezewa visivyo nje ya kisanduku.

Zoo ilipata bao lake kupitia kwa kichwa cha Collins Neto baada tu ya kipindi cha pili kuanza kutokana na kona kabla ya Makwata kupata bao lake la pili dakika ya 67.

Odhiambo alichezewa vibaya nje ya kisanduku kabla ya nahodha Robinson Kamura kuchota frikiki kali iliyotemwa na kipa wa Zoo na kupatia Makwata fursa nzuri ya kutikisa nyavu tena.

Makwata aliongeza bao la nne baada ya kusalia pekee yake na kipa dakika ya 76 na kuwa mchezaji wa kwanza kufungia Ingwe mabao matatu katika mechi moja ligini tangu mwaka 2010.

Ushindi huu ulikuwa wa kwanza wa Ingwe dhidi ya tangu Septemba 2017 iliposhinda 3-1. Tangu wakati huo, timu hizi zilikuwa zimetoka sare mara tatu pamoja na Ingwe kuzabwa 1-0 Januari mwaka 2019.

Uwanjani Afraha mjini Nakuru, wenyeji Ulinzi walilemea Rangers kupitia mabao ya Enosh Ochieng’ na Oscar Wamalwa.

Wanajeshi wa Ulinzi waliona lango kupitia Ochieng’ dakika ya 33 baada ya Daniel Waweru kummegea krosi nzuri.

Oscar Wamalwa alihakikishia Ulinzi ushindi huo wa kwanza katika mechi tano dhidi ya Rangers alipofuma bao la pili dakika ya 85.

Alipokea pasi kutoka kwa Boraafya Omar baada ya ngome ya Rangers kufanya masihara.