Michezo

Ingwe yawapiga Wazito, ila kwa kijasho

March 14th, 2018 1 min read

Na CECIL ODIONGO
KLABU ya AFC Leopards Jumatano imewapa onyo washiriki wengine kwenye ligi kwamba kikosi chao kinahesabiwa miongoni mwa vikosi vyanavyowania Ubingwa wa kipute cha KPL kwa kuwachabanga 3-2  limbukeni Wazito FC.
Wanaingwe ambao kufutia matokeo hayo wamechupa hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la ligi wana pengo la alama sita likiwatenganisha na viongozi wa ligi mabingwa watetezi Gor Mahia ingawa bado wana mchuano mmoja ya kuwajibikia.
Mechi hiyo iliyosakatwa uwanjani Kenyatta Kaunti ya Machakos ilishuhudia kikosi cha Leopards kikisakata kabumbu iliyokwenda skuli na kutikisa mno safu ya ulinzi ya wapinzani wao.
Wazito walichukua uongozi mara mbili kabla ya kuzidiwa mbinu na Ingwe na kumaliza kipute hicho wakiwa wachezaji kumi baada ya mchezaji wao Kevin Ayako kulishwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mlinzi wa Ingwe Moses Mburu.
Hata hivyo kipa wa Klabu ya Wazito Peter Odhiambo alionyesha umahiri wake langoni alipopangua mikwaju miwili ya penalti iliyochanjwa na Mshambulizi Ezekiel Odera na Kiungo Victor Majid.
Mabao ya Ingwe yalifumwa wavuni na Washambulizi Ezekiel Odera na Whyvone Isuza aliyetinga mawili huku Wazito wakifungiwa mawili na mchezaji Pistone Musamba.
Mechi kati ya timu hizo mbili ilifaa kusakatwa kama mchuano wa pili wa kufungua msimu lakini ikaaihirishwa kutoka na AFC kuwajibikia soka ya Barani,CAF dhidi ya klabu ya Fosa Juniours kutoka Kisiwa Cha Madagascar.
Leopards walibanduliwa nje ya mashindano hayo baada ya kulazimisha sare ya 0-0 ugenini na 1-1 nyumbani.