Michezo

Injera na wenzake kupimwa tena corona kabla ya kushiriki Raga ya Dunia

October 31st, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Wanaraga wa Kenya Collins Injera na Andrew Amonde na kikosi chote cha SX10 watapimwa tena virusi vya corona hapo Novemba 2 kabla ya kushiriki Raga ya Dunia ya wachezaji 10 kila upande (World Tens Series) yanayoendelea nchini Bermuda.

Timu ya SX10 kutoka Cape Town nchini Afrika Kusini, ambayo pia imejumuisha Willy Ambaka, Oscar Ouma na Oscar Dennis kutoka timu ya taifa ya Kenya na wachezaji kutoka Afrika Kusini na Ireland ilishuhudia kisa kimoja cha mchezaji kupatikana na virusi vya corona na kutengwa ili kuzuia maambukizi.

Kikosi chote cha SX10, ambacho kinanolewa na raia wa Afrika Kusini Frankie Horne, kimekuwa kikifanya mazoezi mbali na washiriki wengine, huku mchezaji aliyepatikana na virusi hivyo akiwa karantini.

Injera na Amonde wamethibitisha kuwa SX10 imekuwa ikifanya mazoezi ikisubiri raundi ya pili kwa kuchapisha picha wakiwa mazoezini.

Ripoti kutoka Bermuda zinasema kuwa makala hayo ya kwanza yalifaa kuingia raundi ya pili hapo Oktoba 31 na Novemba 1, lakini yamesukumwa hadi Novemba 2 na Novemba 3 ili kupatia timu ya SX10 fursa ya kuyashiriki baada ya kusafiri maelfu ya kilomita kutoka barani Afrika kuhudhuria.

“Kila mtu katika timu ya SX10 atapimwa tena Novemba 2 jinsi masharti ya afya ya Bermuda yanavyosema kuhusu udhibiti wa maambukizi ya virusi vya corona. Wataruhusiwa kucheza ikiwa tu wote watapatikana hawana virusi hivyo,” Afisa Mkuu Mtendaji wa mashindano hayo Jon Phelps alinukuliwa na tovuti ya mashindano hayo akisema.

SX10, ambayo ilipoteza mechi zake zote sita za raundi ya kwanza kwa alama 6-0 dhidi ya kila mpinzani, imeratibiwa kumenyana na Asia Pacific Dragons na London Royals hapo Novemba 2 jioni halafu ipepetane na Rhinos, Phoenix, Ohio Aviators na Miami Sun mnamo Novemba 3. Nusu-fainali na fainali ni Novemba 7.