Habari Mseto

Inspekta Mwala alimuua jamaa wetu, hafai kuachiliwa kwa Sh30,000, familia yalia

September 24th, 2019 2 min read

NA MOHAMED AHMED

FAMILIA ya mwanamume aliyeuawa kwa kugongwa na gari na mwigizaji Davis Mwabili maarufu kama Inspekta Mwala, imegadhabishwa na hukumu hafifu iliyotolewa na mahakama ya Mombasa.

Bw Mwabili, ambaye alimgonga na kumuua Ismael Mangi mwenye miaka 36, hapo Agosti 26 katika barabara kuu ya Kaloleni-Mazeras alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja ama faini ya Sh30,000 kwa kusababisha kifo kutokana na uendeshaji mbaya.

Aidha familia ya mwendazake inadai kuwa siyo haki na hakupewa hukumu inayostahili. Walidai faini aliyopewa ni chini ya Sh40,000 alizopaswa kulipa baada ya kumgonga marehemu Mangi.

Kisa hicho kilitokea eneo la Kwa Randu wakati Bw Mangi alipokuwa akielekea katika kampuni ya simiti ya Rhino ambapo alihudumu kama opareta.

Pia, waliwamalumu maafisa wa polisi kutoka kituo cha Rabai ambako waliandikisha tukio hilo kwamba walitoa baadhi ya taarifa. Kulingana nao, Bw Mwabili anapaswa kukabiliwa na mashtaka makubwa na siyo tu uendeshaji mbaya wa gari.

Babake mwendazake Bw Alex Mangi, aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa maafisa wa polisi walisema hawawezi kuhakiki kuwa mtuhumiwa alikuwa mlevi.

Kulingana na sheria, uendeshaji gari ukiwa mlevi unafaa kutozwa Sh500,000 ama kifungo cha miaka kumi ama yote mawili. Na yeyote atakayesababisha kifo kutokana na uendeshaji mbaya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja ama faini ya Sh100,000.

Familia hiyo haikuridhishwa na jinsi kesi hiyo ilivyosikizwa huku ikisema kuwa Bw Mwabili alifikishwa kortini Septemba 6, siku kumi baada ya tukio hilo kufanyika jambo ambalo wanadai si la kawaida.

Taifa Leo Dijitali ilitaka kujua kutoka kwa Kamanda wa polisi kutoka Rabai, David Maina, lini Bw Mwabili atafikishwa kortini. Afisa huyo alisema atahukumiwa baada ya mwili wa mwendazake kufanyiwa uchunguzi.

Hata hivyo, kulingana na utafiti Taifa Leo iligundua kwamba upasuaji wa maiti ulifanywa siku moja baada ya ajali hiyo.

Kulingana na familia, upasuaji huo ulifanywa Agosti 28 na Dkt Abdhallah kutoka hospitali ya Coast General.

Kabla ya kesi hiyo kupelekwa kotini, fununu zilisema kwamba familia ya mwendazake ilikuwa ikishawishiwa kutatua mzozo huo kinyumbani badala ya kuwasilisha kesi kortini.

Tulipouliza iwapo mpango wa kusuluhisha nje ya koti ulikuwepo, Bw Maina alisema kwamba serikali ilikuwa inaegemea upande wa mshtakiwa.

“Familia haikuwa mlalamishi, ni wananchi kwa niaba yao na kwa sababu ajali ilisababisha kifo, kamwe suala hilo haliwezi kutatuliwa nje ya korti,” alisema Bw Maina.

Mnamo Septemba 9, wakati mshtakiwa alipofikishwa kortini, alikana madai dhidi yake na baadaye kutozwa Sh200,000 ama Sh30,000 pesa taslimu.

Alipofikishwa mbele ya hakimu wa Mariakani, Nelly Adalo , Septemba 19, Bw Mwabili aliitaka mahakama kuyasoma mashtaka dhidi yake upya.

Stakabadhi zilionyesha kuwa mnamo Agosti 26 majira ya saa tatu usiku, mshukiwa aliyekuwa akiendesha gari nambari KCV 807C kutoka Kaloleni kuelekea Mazeras alijaribu kulipita gari pembeni mwa barabara na kisha kukosa mwelekeo na kumgonga msafiri wa mguu na kumsababishia majeraha ya kichwa aliyefariki papo hapo.

Bw Mwabili alikubali mshataka na kuomba kuonewa huruma kwani amekuwa dereva tangu mwaka wa 2007 na hajawai kusababisha ajali.

“Sijawai hata kumgonga mbwa. Ilikuwa ajali na sikuwa na nia ya kufanya ajali hiyo naomba mnionee huruma,” aliomba Bw Mwabili.

Pia alisema kuwa alikuwa anapanga kuitembelea familia ya mwendazake kutoa rambirambi zake na kuifariji.

Bi Adalo alisema kuwa hukumu yake ilizingatia aina ya makosa aliyofanya.

Imetafsiriwa na Fatuma Bugu