Bambika

Instagram ilinipa mume, asema Rev Lucy Natasha

April 18th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MHUBIRI wa kanisa la Empowerment Christian Church, mjini Nairobi, Bi Lucy Natasha, amefichua kuwa alipatana na mumeweStanley Carmel, kwa mara ya kwanza kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram.

Bi Natasha alikiri kuwa iwapo mitandao ya kijamii haingekuwepo, basi hangepata mume. Wawili hao, walipendana kwa muda mfupi na baadaye wakafunga ndoa.

“Unaweza ukapatana na mpenzi wako mtarajiwa kwa njia za ajabu kabisa. Ninamshukuru Mungu kwa uwepo wa mitandao ya kijamii kwa sababu hapo ndipo tulipokutana kwa mara ya kwanza kabisa. Aliingia kwenye DM pale Instagram,” alisema Bi Natasha.

Mhubiri huyo alidai Bw Carmel alimtumia ujumbe ila alimjibu baada ya miaka miwili.

“Nilipojibu ujumbe huo alikuja na mistari ya kuniombea na kunitakia safari njema kila ninaposafiri. Aliniambia ninaonekana vizuri niendelee kung’aa…Lakini ilinichukua muda mrefu kuona jumbe zake kwa sababu kuna watu wengi waliokuwa wakinifuata mtandaoni,” alisema Natasha.

Mojawapo ya video zake ziliweza kusambaa, ikiwemo aliyokuwa akihubiri kuhusu familia ya kifalme, iliyompa fursa ya mumewe kuanza kumfuata mitandaoni na kuzidi kumtumia jumbe za kumtia moyo kwa kazi anayofanya.

“…Kutoka hapo akaendelea kuniandikia jumbe za endelea kung’aa, endelea kupeleka watu kwa Mungu. Lakini hakuwahi andika ujumbe kwamba “nakupenda”.

“Baada ya miaka miwili, nikasema acha nimuangalie huyu ni nani halafu nikamjibu, kama vile nilianzisha mazungumzo,” alieleza Natasha.

Baada ya hapo, Natasha alisema kuwa walikuja kukutana nchini Marekani, jimbo la Texas ambapo kila mmoja alikuwa amealikwa kivyake kwa mikutano tofauti ya injili.

Kwa sasa, mhubiri huyo na nabii Carmel wameishi kwenye ndoa yao takriban miaka miwili.