Inter Milan yadidimiza matumaini ya Barcelona kutinga hatua ya 16-bora UEFA

Inter Milan yadidimiza matumaini ya Barcelona kutinga hatua ya 16-bora UEFA

Na MASHIRIKA

KOCHA Xavier Hernandez amesema kikosi chake cha Barcelona kilidhulumiwa na refa katika mchuano wa Kundi C kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uliosakatiwa uwanjani San Siro, Italia, mnamo Jumanne usiku.

Matokeo hayo yalisaza Barcelona katika hatari ya kutofuzu kwa hatua ya 16-bora ya kipute hicho kwa mara ya pili mfululizo.

Bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo lilifungwa na Hakan Calhanoglu mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Barcelona walidhani walikuwa wamesawazishiwa na Pedri katika kipindi cha pili ila goli lake likafutiliwa mbali na refa baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kuwa alifunga kutokana na mpira ambao Ansu Fati alikuwa ameunawa awali.

Kichapo hicho kiliacha Barcelona katika nafasi ya tatu kwenye Kundi C kwa alama tatu, tatu nyuma ya nambari mbili Inter na sita nyuma ya Bayern Munich waliokomoa Viktoria Plzen ya Jamhuri ya Czech 5-0 nchini Ujerumani.

Inter na Barcelona walishuka dimbani kila mmoja akiwa amecharaza Viktoria Plzen na kutandikwa na Bayern. Huku Inter wakishuhudia mwanzo mbaya zaidi katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) tangu 2011, Barcelona hawajapoteza mechi yoyote kati ya saba zilizopita katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kichapo cha 2-1 kutoka kwa AS Roma ugani San Siro wikendi iliyopita kilikuwa cha kwanza kwa Inter kupokea kutoka kwa kikosi hicho tangu 2017. Matokeo hayo yaliacha Inter katika nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 12 baada ya kushinda mechi nne na kupiga sare nne kutokana na mechi nane zilizopita za Serie A.

Baada ya kufungua kampeni za UEFA kwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Bayern, Inter walisajili ushindi sawa na huo dhidi ya Plzen. Barcelona kwa upande wao waliponda Plzen 5-1 ugani Camp Nou kabla ya Bayern kuwanyuka 2-0 jijini Munich.

Hadi kufikia Jumanne, Inter walikuwa wamewahi kushinda Barcelona mara moja pekee kutokana na mechi tano za awali jijini Milan. Barcelona walibanduliwa kwenye makundi ya UEFA mnamo 2021-22, hiyo ikiwa mara yao ya nne katika historia. Aidha, ilikuwa mara yao ya kwanza tangu 2000-01 kuaga kivumbi hicho katika hatua za mapema.

Wakipania kuzima nuksi hiyo, Barcelona walijisuka upya msimu huu na wana kiu ya kurejesha hadhi yao kwenye soka ya Uhispania na bara Ulaya. Waliweka mezani zaidi ya Sh19 bilioni ili kujinasia huduma za wachezaji saba, akiwemo Lewandowski aliyefungia Bayern mabao 344 kutokana na mechi 375. Walinyanyua taji la UEFA mara ya mwisho mnamo 2014-15 baada ya kufinya Juventus ya Italia 3-1 jijini Berlin, Ujerumani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Tottenham na Frankfurt waumiza nyasi bure katika pambano la...

Uhalalishaji wa GMO wazua mjadala mkali

T L