Michezo

Inter Milan yafichua mpango wa kumng'oa Aguero uwanjani Etihad

October 19th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

INTER Milan wamefichua azma ya kumsajili fowadi matata wa Manchester City na timu ya taifa ya Argentina, Sergio Aguero, bila ada yoyote baada ya mkataba wake wa sasa na kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kukamilika rasmi mnamo Juni 2021.

Kocha Antonio Conte amepania kumtwaa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 32 kwa matarajio kwaamba atawezesha Inter Milan kukomesha ukiritimba wa Juventus kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Ingawa hivyo, kubwa zaidi katika maazimio ya Conte, ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Chelsea, ni kuwapigisha Inter hatua kubwa zaidi kwenye soka ya bara Ulaya baada ya kuzidiwa maarifa na Sevilla kwenye fainali ya Europa League msimu jana.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, Inter wapo radhi kumpokeza Aguero mkataba wa awali wa miaka miwili kabla ya kurefusha kandarasi yake kwa mwaka mmoja zaidi iwapo atawaridhisha wasimamizi wa kikosi.

Gazeti la Calcio Mercato nchini Italia limefichua kwamba Inter watakuwa wakimpokeza Aguero mshahara wa kati ya Sh895 milioni na Sh1 bilioni kwa mwaka; na huenda makubaliano hayo yakafikiwa mwishoni mwanzoni mwa Januari 2021.

Aguero ambaye kwa sasa ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Man-City anatazamiwa kuwa kizibo kamili cha fowadi Lautaro Martinez ambaye anatarajiwa kuyoyomea Uhispania na kuingia katika sajili rasmi ya Barcelona mnamo Januari mwaka ujao.

Aguero alisajiliwa na Man-City mnamo 2011 baada ya kushawishiwa kuagana na Atletico Madrid ya Uhispania kwa kima cha Sh4.9 bilioni. Tangu wakati huo, amekuwa tegemeo kubwa ugani Etihad na ameshindia Man-City mataji manne ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), matano ya League Cup na Kombe la FA mara moja.

Katika kampeni za msimu uliopita, Aguero alifungia Man-City jumla ya mabao 23. Hata hivyo, alishindwa kuwaongoza waajiri wake walionyanyua taji la League Cup pekee kuhimili ushindani mkali kutoka kwa Liverpool waliotawazwa mabingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Aidha, Man-City walibanduliwa na Arsenal kwenye nusu-fainali za Kombe la FA na wakadenguliwa na Olympique Lyon ya Ufaransa kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kichapo cha 3-1 jijini Lisbon, Ureno.

Kubwa zaidi ambalo Aguero anakumbukiwa kwalo kambini mwa Man-City ni kufunga bao la dakika za majeruhi dhidi ya Queens Park Rangers (QPR) katika siku ya mwisho ya kampeni za EPL mnamo 2011-12 na kuwanyima Manchester United fursa ya kunyanyua taji hilo.

Nyota huyo ambaye kwa sasa amehudumu kambini mwa Man-City kwa kipindi cha miaka tisa, sasa amepona jeraha ambalo lilimweka nje kwa kipindi cha miezi minne iliyopita.

Aguero alipata jeraha baya la goti mnamo Juni 22, 2020 wakati wa mechi ya EPL iliyowakutanisha na Burnley. Jeraha hilo lilimkosesha mechi zote 10 za mwisho wa muhula wa 2019-20 na pia michuano miwili ya UEFA dhidi ya Real Madrid na Lyon mnamo Agosti.

Kukosekana kwa Aguero katika kikosi cha kwanza cha Man-City kwa kipindi hicho kulimpisha fowadi raia wa Brazil, Gabriel Jesus aliyefunga jumla ya mabao matano kutokana na mechi 12 za mwisho wa msimu uliopita kushirikiana sasa na Raheem Sterling, Phil Foden, Bernardo Silva na Riyad Mahrez kwenye safu ya mbele ya kikosi hicho.

Baada ya kupiga Arsenal 1-0 katika mechi ya EPL mnamo Oktoba 17, 2020, Man-City kwa sasa wanajiandaa kushuka dimbani kwa mechi ya kwanza ya UEFA dhidi ya FC Porto ya Ureno mnamo Oktoba 21.