Michezo

IPO KAZI! Rooney amtaka Ole Gunnar Solskjaer aingie sokoni

June 13th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

NEW YORK, Amerika

NAHODHA wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney anaamini kuwa kikosi kinachoundwa na kocha Ole Gunnar Solskjaer kitakuwa imara na chenye uwezo wa kushindana vikali na timu nyinginezo za Bara Ulaya msimu ujao.

“Klabu inafaa kujengwa na wachezaji wachanga lakini sharti wawe wazuri baada ya kipindi cha miaka miwili kabla ya kuanza kupigania mataji makubwa kama vile ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA),” alisema.

Mwingereza huyo ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya DC United nchini Amerika, anamtaka kocha huyo atafute wachezaji kadhaa wa viwango bora ili timu hiyo ifaulu msimu ujao, badala ya kutumia Sh15 bilioni kuleta mchezaji mmoja.

Rooney anamtaka Ole Gunnar anunue wachezaji watano ama sita kwa kutumia kati ya Sh4.5 bilioni na Sh6 bilioni ili akijenge kikosi chake kutokana nao.

“Unaweza kuleta wanasoka wa majina makubwa kama vile Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Sergio Ramos na Bale lakini itakugharimu Sh52.5 bilioni, lakini baada ya miaka miwili hivi, pesa hizo zitakuwa zimepotea,” alisema mvamizi huyo.

Thamani ya miamba hao inatokana na ufanisi wao. Kwa mfano Messi na Ronaldo wameshinda mataji ya FIFA Ballon d’Or mara 10, huku nahodha wa Real Madrid, Ramos akijivunia ubingwa wa Kombe la Dunia, Ubingwa wa Ulaya (Euro) na mataji manne ya UEFA.

Bale mwenye umri wa miaka 29 ambaye pia huchezea Real, ameshinda taji la UEFA mara nne na kwa kipindi kirefu, amehusishwa na uhamisho wa kujiunga na Man-United. Rooney amesema utakuwa wakati mgumu kwa kocha Ole Gunnar ambaye ameripotiwa kulenga majina makubwa ya kuleta Old Trafford, akiwemo beki matata kinda Matthijs de Ligt wa Ajax Amsterdam.

Ujenzi

Kocha huyo aliyemrithi Jose Mourinho ameanza mipango ya kukijenga kikosi chake baada ya majuzi kumtwaa Daniel James mwenye umri wa miaka 21 kutoka Swansea City. Rooney ambaye aliwahi kuwa mfungaji wa mabao mengi akiichezea Man-United na timu ya taifa ya Uingereza, alisema ataunga mkono kikamilifu mipango ya Ole Gunnar kununua wachezaji chipukizi badala ya kukimbilia wachezaji walio na umri mkubwa.

Starika huyo kadhalika alisema timu kama vile Chelsea, Arsenal, Tottenham na Everton zinahitaji kipindi cha miaka miwili kufikia kiwango cha Liverpool na Manchester City. Wakati uo huo, Rooney anaamini kuwa kushindwa kwa Uingereza na Uholanzi katika michuano ya Uefa Nations League kutasaidia timu hizo kucheza kwa bidii katika mechi zijazo, huku akitumai kuwa kocha Gareth Southgate wa Uingereza ataendelea kuisaidia timu hiyo.

“Kila mtu alisikitishwa na kushindwa kwa kikosi cha Southgate, lakini lazima watu waelewe ni timu ya wachezaji wachanga ambao kocha aliamua kuwapa nafasi,” aliongeza.