Habari

Ipo njama ya kuzima Ruto 2022

December 29th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Aden Duale, amefichua mipango anayodai kuwa inaendelezwa kichinichini katika Serikali ya Jubilee kwa nia ya kumzuia Naibu Rais William Ruto kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Kwa mujibu wa Bw Duale, mtindo uliotumiwa na baadhi ya washawishi serikalini kumzuia Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto kuwania urais wa 2013, ndio umeanza kutumiwa sasa katika serikali kuzima nyota ya Naibu Rais kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Katika uchaguzi huo wa 2013 ilifichuka kuwa palikuwa na kikundi cha watu wenye ushawishi mkubwa ambao walitaka Rais Kenyatta na Dkt Ruto kuweka kando maazimio yao na badala yake kumuunga mkono kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.

Kwenye mahojiano ya kina aliyofanyiwa na gazeti la ‘Sunday Nation’ ambayo yamechapishwa leo Jumapili, Bw Duale alisema kilinge kama hicho kiko katika Serikali ya Jubilee na kinafanya juu chini ili Dkt Ruto asiwe Rais, nia yake ikiwa kumuunga mkono kiongozi wa taifa atakayelinda masilahi yao binafsi.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini ‘aliapa’ kuwa, sawa na jinsi yeye na wenzake walivyozima njama ya kumwingiza Bw Mudavadi mamlakani katika mwaka wa 2013 kwa lazima, ndivyo watakavyofanya mara hii kuhakikisha Dkt Ruto anashinda urais.

“Sawa na ilivyokuwa katika serikali zote zilizotangulia, kuna watu walafi na wabinafsi ambao wanadhani wana mamlaka ya kuamua atakayeingia mamlakani. Ninawapa changamoto wakasome historia hasa ya 2013 wakati Musalia Mudavadi alipofanywa mgombeaji wetu wa urais kwa saa 48,” akasema.

Ijapokuwa hakusema kikundi hicho kinajumuisha kuwa kina nani hasa, alidokeza kwamba baadhi yao ni maafisa wenye ushawishi mkubwa katika serikali ya Rais Kenyatta wakiwemo mawaziri.

Alidokeza pia kwamba watu hao wangependa mmoja wa wanasiasa walioshindwa kwenye chaguzi zilizopita ndiye awe Rais ifikapo 2022 badala ya Dkt Ruto.

Miongoni mwa viongozi ambao wadadisi wa kisiasa husema huenda wakaungwa mkono na serikali ya Rais Kenyatta kuwania urais ujao ni Kiongozi wa ODM Raila Odinga, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka na Bw Mudavadi.

Hivi majuzi, Bw Musyoka alisema wazi kwamba atafuata msimamo utakaochukuliwa na Rais Kenyatta kuhusu ugombeaji urais.

Isitoshe, bwanyenye Peter Muthoka aliyefadhili kampeni za Rais Kenyatta na Jubilee katika miaka ya 2013 na 2017, alihudhuria mkutano wa viongozi wa Ukambani ulioitishwa na Bw Musyoka, akamwaga mamilioni ya pesa zilizogawanywa kwa wanasiasa na viongozi wa dini waliohudhuria wiki iliyopita.

Kwa upande mwingine, urafiki wa Rais Kenyatta na Bw Odinga kisiasa umezidi kunawiri tangu walipoweka mwafaka wa maridhiano (BBI) mwaka uliopita na hatimaye wakazindua ripoti ya jopo la maridhiano mwaka 2019.

Licha ya hayo, Bw Duale bado anaamini Rais Kenyatta atamuunga mkono naibu wake ifikapo 2022 kwani hajatangaza hadharani kama alibadili ahadi aliyomtolea hasa katika hatamu yake ya kwanza.

“Walio kati yetu ambao ni watu wenye heshima zao, waadilifu na wanaomcha Mungu, tutasimama kidete na Naibu Rais hadi mwisho ili awe rais wa tano wa Kenya. Amehitimu kuongoza nchi hii licha ya jinsi wengine wanavyokusanya watu walioshindwa na kukataliwa katika chaguzi zilizopita,” akaeleza.

Alidai kwamba mipango hiyo yote ya kumpiga vita Dkt Ruto inaendelezwa kwa ufadhili wa pesa za umma kupitia wizara mbalimbali.

Bw Duale alipuuzilia mbali ripoti kwamba Chama cha Jubilee kimesambaratika, akisema wataanza kujiandaa kikamilifu kwa uchaguzi wa 2022 mwaka 2020.

Hata hivyo, alitilia shaka nia ya handsheki akisema haijafanikiwa kuleta maridhiano bali imeyumbisha Jubilee na Muungano wa NASA kwa kiasi cha kugawanya Wakenya zaidi.