Michezo

Ipo siku Manchester City itatwaa kombe la Uefa, Guardiola asisitiza

June 12th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amesema baada ya kushinda mataji mawili mfululizo ya ligi kuu ya Uingereza (EPL) na mengine ya FA Cup na Carabao Cup, sasa analenga ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (Uefa).

Mkataba wa Mhispania huyo na klabu hiyo ya Etihad unafikia tamati Juni 2021 baada ya kuongeza muda wa kukinoa kikosi hicho, lakini amesema kama si msimu ujao, atajaribu msimu unaofuata kushinda taji hilo.

“Manchester City inaweza kutwaa ubingwa wa Uefa msimu ujao nikiwepo au nisipokuwepo. Pengine itashinda na wachezaji hawa wa sasa au watakaokuja baadaye, muhimu ni kwamba tunaamini ipo siku tutashinda taji hili,” alisema Guardiola.

Kocha huyo kadhalika alipuuza madai kwamba huenda akaondoka hivi karibuni na kujiunga na klabu nyingine baada ya taji hilo la Uefa kumponyoka mara kadhaa.

“Hapa nilipo kwa sasa ni mahali pazuri pa kufanya kazi, na ningependa kuwahakikishia mashabiki kwamba nitaendelea kuwa hapa Etihad kwa angalau misimu miwili ijayo,” aliongeza.

“Kwa hakika, Uingereza ndio sehemu nzuri zaidi ya kufanya kazi ya ukufunzi. Ni sawa na Uhispania na Ujerumani, kwani sijawahi kwenda mataifa mengine kama Italia. Mashabiki hapa wameniunga mkono kikamlilifu,” alisema.

“Nakumbuka mwaka wa kwanza ulikuwa mgumu, hasa baada ya kushindwa na Monaco katika Ligi ya Mabingwa na pia wakati huo hatukuwa vizuri katika ligi kuu ya Uingereza (EPL). Lakini mashabiki waliendelea kusubiri.

Utulivu

Guardiola aliwapongeza mashabiki wa Manchester City kwa kuwa watulivu hata wakati matokeo yakiwa duni.

“Kuna utulivu wa hali ya juu katika klabu hii. Sijajua mambo yalivyo kwingineko. Nipo tayari kuhudumu hapa kwa misimu mwili zaidi baada ya kuipa klabu hii mataji matano kwa muda wa misimu mitatu, kwa sababu wengi wanasubiri ubingwa wa Uefa,” aliongeza.

Tangu ajiunge na klabu hii, Guardiola hajawahi kuvuka hatua ya robo-fainali katika michauno hiyo ambapo msimu uliopita walipigwa breki na Tottenham na waliowang’oa kwenye hatua hiyo.

Katika msimu wa kwanza, walishindwa na Monaco katika hatua ya 16 Bora.

Wakati huo huo, beki wa Juventus na kikosi cha Ureno, Joao Cancelo mwenye umri wa miaka 25 anatazamiwa kujiunga na Manchester City kwa kitita cha Sh6.6 bilioni.

Lakini hiyo itawezekana tu iwapo klabu hiyo ya EPL itafanikiwa kuachana na beki Danilo raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 27.