Habari Mseto

IPOA kuchunguza polisi aliyeua watu 5 na kuwajeruhi wengine

December 18th, 2018 2 min read

NA GERALD BWISA

AFISA wa Polisi anayedaiwa kuua watu watano na kuwajeruhi wengine katika kijiji cha Kolongolo, eneobunge la Kwanza, Kaunti ya Trans-Nzoia amekamatwa na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kitale.

Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) ilisema imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho, huku Inspekta Mkuu wa Polisi, Bw Joseph Boinnet akitetea maafisa wake na kusema maisha yao yalikuwa hatarini.

Tukio hilo lilitokea Jumapili mwendo wa saa kumi jioni wakati maafisa watatu wa polisi walipokuwa wakijaribu kutatua ugomvi wa kinyumbani katika boma moja eneo hilo.

Inasemekana maafisa hao walifika katika makazi ya mshukiwa na zogo likatokea alipokataa kutiwa nguvuni huku marafiki zake wakilalamikia jinsi polisi walivyokuwa wakimhangaisha wakitaka kumtia pingu.

Hapo ndipo polisi mmoja alitoa bunduki yake na kuwapiga risasi watu wawili waliofariki papo hapo.

“Maafisa hao walikuwa wameenda kumkamata mwanaume kwa jina Dan Juma ambaye anadaiwa alimpiga mkewe Metrin Shikuku lakini akakataa kutiwa pingu,” Kamishna wa Kaunti hiyo, Bw Erastus Mbui alieleza.

Spika wa kaunti hiyo, Bw Joshua Werunga alikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo Kamishina wa Kaunti ya Trans Nzoia Erastus Mbui hangeweza kuthibitisha ikiwa watu wengine watatu waliojeruhiwa na kulazwa kutokana na majeraha ya risasi kwenye hospitali mbalimbali mjini Kitale pia walifariki.

“Idadi ya waliofariki iliyothibitishwa na polisi ni wawili ingawa kuna ripoti kwamba wengine watatu wameaga dunia kwenye hospitali mbalimbali walikolazwa,” akasema Bw Mbui.

Kulingana naye, ugomvi mkubwa ulitanda baada ya wenyeji kuwazuia polisi kumkamata mwanaume aliyedaiwa kumwangushia mkewe kipigo kikali.

“Maafisa hao walikuwa wameenda kumkamata mwanaume kwa jina Dan Juma ambaye anadaiwa alimpiga mkewe Metrin Shikuku lakini akakataa kutiwa pingu,” akasema Bw Mbui.

Kufuatia mauaji hayo, wenyeji waliwapiga kwa mawe maafisa hao na ndipo wakawafyatulia risasi.

Spika wa kaunti hiyo Joshua Werunga ambaye alikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa alifikishwa katika hospitali ya Kitale kufanyiwa huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa kwa matibabu zaidi hadi hospitali ya Mafunzo na rufaa ya Eldoret. Bw Werunga alipigwa kwa kifaa butu.

Majeruhi wengine 10 nao wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za rufaa za Kitale na Mt Elgon.