IPOA yaripoti ongezeko la idadi ya malamishi dhidi ya polisi

IPOA yaripoti ongezeko la idadi ya malamishi dhidi ya polisi

Na CHARLES WASONGA

IDADI ya malalamishi yanayowasilishwa na umma dhidi ya maafisa wa polisi iliongezeka kwa kiwango cha asilimia 83.4 ndani ya miaka kumi iliyopita.

Hii ni kulingana na ripoti ya hivi punde iliyowasilishwa na Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) katika bunge la Seneti.

Kulingana na ripoti hiyo, malalamishi hayo yameongezeka kutoka 594 mnamo mwaka wa 2011 hadi 3,583 mnamo mwaka huu wa 2021.

Miongoni mwa malalamishi hayo, 22 yaliwasilishwa IPOA ndani ya kipindi cha janga la Covid-19.

Nyingi za kesi hizo ni vifo kutokana na dhuluma zilizotekelezwa na polisi, watu kupotezwa kwa njia tata, uhalifu wa kingono, polisi kutowajibika, matumizi mabaya ya mamlaka ya polisi na visa vya polisi kuwajeruhi na kuwatesa watu.

“Ndani ya kipindi hicho, IPOA iliendesha chunguzi 956. Faili 200 za uchunguzi ziliwasilishwa kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ili zishughulikiwe. Kwa upande mwingine, kesi 98 zilikuwa mbele ya mahakama kufikia Juni 30, 2021,” ripoti hiyo ikasema.

Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori ambaye alifika mbele ya Kamati ya Pamoja ya Seneti kuhusu Haki na Sheria na ile ya Usalama alisema utendakazi wa tume yake umeimarika tofauti na miaka ya nyuma.

“Kesi ambazo tunachunguza kwa wakati mmoja zimeimarika kuanzia 27 mamlaka hii ilipoasisiwa hadi kesi 956 kufikia Juni 2021. Hii inaonyesha wazi kuwa utendakazi wetu umeimarika kwa kiwango kikubwa mno,” Bi Makori akaeleza.

Mwenyekiti huyo alikuwa amefika mbele ya maseneta wanachama wa kamati hizi mbili kujibu maswali kuhusu mienendo ya polisi wanapotekeleza kanuni za kuzuia maambukizi ya corona, ambayo imechangia maafa mengi.

Maseneta wanaendesha uchunguzi kuhusu vifo vya kaka wawili wa kule Kianjokoma katika Kaunti ya Embu mwezi Agosti. Wao ni Benson Ndwiga aliyekuwa na umri wa miaka 22, na Emmanuel Ndwiga aliyekuwa na umri wa miaka 19.

Inadaiwa kuwa vijana hao ambao walikuwa wanafunzi wa chuo kikuu walifariki mikononi mwa maafisa wa polisi waliowakamata kwa kukiuka sheria za kafyu.

  • Tags

You can share this post!

Mjukuu wa Moi adai hana uwezo kulea watoto

Nimerejea Manchester United izaliwe upya – Ronaldo