Habari Mseto

IPSOS: Wakenya wamsifu Kalonzo kama asiye na doa la ufisadi

August 23rd, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, hana doa la ufisadi ikilinganishwa na viongozi wengine wa kisiasa, kwa mujibu wa utafiti.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Ipsos ilionyesha asilimia moja pekee ya Wakenya ndio wanaamini Bw Musyoka ni mfisadi.

Vile vile, Rais Mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walitajwa na asilimia tano pekee ya Wakenya kujihusisha na ufisadi.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Julai 25 na Agosti 2 ulinuia kubaini wanavyodhani ama kujua kuhusu ufisadi nchini na matokeo yake yalitolewa jana.

Akitoa matokeo hayo katika makao makuu ya Ipsos, Lavington Jijini Nairobi Jumatano, mtafiti mkuu wa kampuni hiyo Prof Tom Wolf aidha alisema Wakenya wengi hawaamini kuwa wakubwa kwenye serikali na wafanyabiashara wenye umaarufu watahukumiwa.

“Ni asilimia 17 pekee ya Wakenya ambao wanaamini kuwa kuna uwezekano kwa wale wanaochukuliwa kuwa ‘samaki wakubwa’ kuhukumiwa, huku asilimia 73 wakiamini hilo haliwezekani,” akasema Prof Wolf.

Kulingana na utafiti huo vilevile, bado asilimia 35 ya Wakenya haiamini kuwa Rais Uhuru Kenyatta amejitolea kikamilifu kupigana na ufisadi, asilimia 27 yao wakiwa wafuasi wa chama chake cha Jubilee. Ni asilimia 21 pekee wanaoamini kwa uhakika kuwa Rais Kenyatta atafaulu kupunguza ufisadi nchini, huku 31 wakidhani tu ila bila kuwa na uhakika kuwa atafaulu.

Asilimia 17 ya waliohojiwa walisema haonyeshi dalili ila kuna uwezekano, huku asilimia 24 wakiwa na hakika kuwa hatafaulu.

Wengi wa waliohojiwa walitaja suala la kujihusisha na uongozi wa kisiasa na vitisho kutoka kwa watu wenye umaarufu, kama kikwazo kikuu cha vita dhidi ya ufisadi nchini.

“Jambo la kushangaza ni kuwa asilimia nne ya Wakenya wanadhani kuwa hakuna chochote kitakachofanywa chaweza kumaliza ufisadi Kenya,” akasema mtafiti huyo.

Lakini asilimia 31 walipendekeza adhabu kali zaidi kwa wanaopatikana na hatia, 23 wakimtaka Rais kuwapiga kalamu wale wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi nao asilimia 17 wakipendekeza uhamasisho zaidi kwa umma.