Kimataifa

Iran kuendelea kupambana na Amerika, ubalozi wasema

January 9th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

UBALOZI wa Iran nchini Kenya umekariri msimamo wa serikali ya nchi hiyo kwamba itaendelea kufanya mashambulio ya kulipiza kisasi dhidi ya Amerika kwa kuua Luteni Jenerali Qasem Soleimani ambaye alikuwa akiongoza operesheni za kijeshi za Iran nchini Iraq na eneo zima la Mashariki ya Kati.

Katibu katika ubalozi wa Iran, ambaye pia ndiye mkuu wa kitengo cha kisiasa Tohid Afzali, Jumatano aliwaambia wanahabari jijini Nairobi kwamba nchi yake iko tayari kujitetea dhidi ya kile alichokitaja kama “uchokozi kutoka kwa Amerika.”

Afzali aliwataja wanajeshi wa Amerika kama ‘kundi la magaidi’ ambalo linajifanya kupambana na jinamizi hilo kwa kuendesha vitendo vya ukiukaji wa Sheria za Kimataifa ambazo zinatambuliwa na Umoja wa Mataifa.

“Hatua hii ya uchokozi ililenga kuzidisha uhasama na taharuki katika eneo la Mashariki ya Kati ambalo tayari linakabiliwa na changamoto nyingi. Hii ni ithibati tosha kwa Amerika italipia hasara zote zinazotokana na vitendo kama hivyo,” akasema.

Mnamo Jumatatu Kiongozi wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliapa kwamba nchini yake itaendelea kufanya mashambulio ya kulipiza kisasa dhidi ya Amerika.

Na mnamo Jumatano Iran ilifanya mashambulio kadhaa ya roketi katika kambi mbili za wanajeshi wa Amerika nchini Iraq.

Roketi hizo zilirushwa katika kambi ya Ain al-Asad iliyoko mkoa wa Anbar na ile ya Erbil majira ya asubuhi huku uhasama kati ya Iraq na Amerika ukionekana kuendelea kutokota.

Luteni Jenerali Soleimani aliuawa wiki jana katika shambulio lililotekelezwa na droni nchini Iraq, kufuatia agizo la Rais Donald Trump. Rais huyo wa Amerika alimtaja Luteni huyo kama mtu hatari ambaye amekuwa akifanya mashambulio ya kulenga raia wa Amerika na wanajeshi wake walioko nchini Iraq.

“Jeneral Qasem Soleimani ameuawa katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa nan a Amerika ilhali alikuwa amealikwa rasmi na Waziri Mkuu wa Iraq kuwasilisha majibu ya Iran kwa Saudi Arabia,” akasema.

Hata hivyo, Trump amekana madai kuwa nchini yake itataka kuchochea vita zaidi na taifa hilo la ghuba la Uajemi.

Badala yake, Rais huyo wa Amerika alisema shambulio lililotekelezwa na wanajeshi wa Amerika lililenga kuzuia mashambulio ya Iran.