Kimataifa

Iran yafananisha shambulio la Israel na ‘kalongolongo’

April 20th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

TEHRAN, IRAN

SERIKALI ya Iran imedunisha shambulio lililotekelezwa na Israel mnamo Ijumaa, huku ikilirejelea kama hafifu na linalofanana na mchezo wa mwanasesere.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian akihojiwa Ijumaa alisema kwamba shambulio hilo ni kama mchezo wa ‘kalongolongo’.

“Shambulio hilo lilikuwa ni kama kazi ya bure. Ndege zao zisizo na rubani ni kama vifaa ambavyo watoto wetu wanatumia kucheza,” akasema waziri Amir-Abdollahian katika mahojiano.

Hata hivyo, waziri huyo alisema kwamba serikali yao ingechukua hatua ya haraka iwapo shambulio la Israel lingeleta madhara kwa nchi yao.

“Shambulio hilo lingeleta maadhara kwetu, basi tungechukua hatua ya haraka kulijibu,” Amir-Abdollahian alisema katika mahojiano ya Ijumaa.

Hata hivyo, alisisitiza Iran itachukua hatua za kijeshi kulipiza shambulio la Israel.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Israel kukaidi wito wa kutolipiza kisasai na kuishambulia Iran.

Ijumaa, sauti ya makombora ilisikika katika mji wa Isfahan katikati mwa Iran.

Naye Waziri mwenye msimamo mkali wa Usalama wa Israel, Itamar Ben-Gvir, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, kwamba shambulio hilo lilikuwa ‘dhaifu’ na ndogo mno.

Amerika na washirika wengine wa nchi za magharibi wamekuwa wakiitaka Israel isitishe mashambulio yake ya kijeshi ili kuepusha mzozo wa kikanda unaotokana na vita vya Israel na Hamas.

Iran ilishambulia Israel Jumamosi kujibu shambulio lililotekelezwa na Israel katika ubalozi wake jijini Damascus nchini Syria mnamo Aprili 1, 2024.

Ingawa shambulio la Iran halikusababisha vifo, baada ya wanajeshi wa Israeli na washirika wake kudungua makombora hayo, limeibua hofu ya kuenea kwa vita vinavyoendelea Gaza.

Aidha, kuna wasiwasi kwamba huenda vita kamili vikazuka kati ya Israel na hasidi wake wa muda mrefu Iran.

Tangu vita vilipoanza Gaza Oktoba mwaka jana, mapigano yametokea kati ya Israel na makundi washirika wa Iran, yaliyoko Lebanon, Syria, Yemen na Iraq.

Mapema Jumatatu, nchi za bara Uropa, ambazo ni washirika wa Israel, ziliihimiza kujizuia na kutotekeleza mashambulio ya kulipiza kisasi Iran.

Nchi hizo–Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani–ziliendelea kuhimiza, sawa na Amerika pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres, viongozi wa Israel kujiepusha na hatua hiyo itakayozidisha mapigano katika eneo la Mashariki mwa Kati.