Kimataifa

Iran yaishambulia Israeli kwa msururu wa droni

April 14th, 2024 1 min read

REUTERS Na WANDERI KAMAU

Jerusalem, Israeli

IRAN mnamo Jumamosi, Aprili 13, 2024 usiku ilizindua msururu wa mashambulizi ya droni na makombora dhidi ya Israeli, kwenye shambulio la ulipizaji kisasi lililoripotiwa kumjeruhi msichana wa miaka saba.

Ripoti nchini Israeli zilisema mashambulio hayo pia yalisababisha uharibifu mdogo dhidi ya kituo kimoja cha kijeshi.

Droni hizo zilirushwa katika miji mikuu kadhaa kama Tel Aviv na Jerusalem Magharibi.

Milipuko mikubwa ilisikika wakati droni na makombora hayo yalizimwa na mitambo maalum ya kijeshi kudhibiti mashambulio kama hayo.

Jeshi la Israeli lilisema mashambulio hayo yalijumuisha “zaidi ya droni na makombora 300”.

“Hata hivyo, mitambo yetu ilifanikiwa kuzima asilimia 90 ya makombora hayo,” likasema jeshi hilo Jumapili, Aprili 14, 2024.

Jeshi hilo pia lilipata usaidizi kutoka kwa mataifa kama Ufaransa, Uingereza na Amerika kuzima droni hizo.

Kando na Iran, jeshi hilo lilisema kuwa droni hizo zilirushwa kutoka mataifa mengine kama Iraq na Yemen.

Wahudumu wa afya walisema kuwa msichana mmoja Kusini mwa Israeli alijeruhiwa na kipande cha droni iliyozimwa na mitambo maalum.

“Tulibaini droni kadhaa zilizorushwa katika kituo kimoja cha kijeshi eneo la Kusini na kusababisha uharibifu mdogo,” likasema jeshi.

Kundi la Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) kutoka Iran lilithibitisha kutekeleza shambulio hilo.

Lililitaja kama “ulipizaji kisasi dhidi ya shambulio la Israeli kwa ubalozi wake nchini Syria mnamo Aprili 1, ambapo watu 12 waliuawa”.

Hadi sasa, Israeli haijathibitisha au kukana kuhusu ikiwa ilihusika kwenye shambulio hilo.

Mnamo Jumapili, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, alitangaza “ushindi” dhidi ya Iran na washirika wake.