Kimataifa

Iran yamnyonga shoga mbele ya umma

January 31st, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAUME wa miaka 31 kutoka Iran alinyongwa mbele ya umma, baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka sheria yake ambayo hairuhusu ushoga na kuteka nyara watoto.

Mwanaume huyo alinyongwa mnamo Januari 10 katika Jiji la Kazeroon, kusini mwa taifa hilo, aliposhtakiwa na kosa la kufanya ngono na mwanaume mwenzake.

Kosa la ushoga huadhibiwa kwa kifo nchini humo, ambapo sheria ya sharia hutumika.

Mwanaume huyo aliripotiwa kuteka nyara wavulana hao wa miaka 15, japo haikufafanuliwa ikiwa ni wao ambao aliwalawiti.

Raia wa jiji hilo baadaye waliripotiwa kusherehekea hatua hiyo ya korti kumhukumu kifo, wakisema waliridhika.

Kufuatia kisa hicho, watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja Iran wanasemekana kuishi kwa woga. “Wamekuwa wakiishi kwa hofu kwa miaka 40 iliyopita,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya New Iran ya Kimarekani Alireza Nader.

Kulingana na ufichuzi wa 2008 wa kampuni ya British Wikileaks, kati ya 1979 na 2008, Iran ilikuwa imeua mashoga 4,000 na wasagaji 6,000.

Mvulana wa miaka 19 Hassan Afshar alinyongwa katika jela ya Arak, mkoa wa Markazi mnamo Julai 18, 2016, aliposhtakiwa kwa kufanya ngono ya lazima na mwanaume mwingine mnamo 2015.

Mnamo 2011, serikali ya Iran aidha iliua wanaume watatu raia wake walipopatikana na hatia ya makosa yaliyohusiana na mapenzi ya jinsia moja.