Michezo

Ireland sasa yaita Maguire na Horgan kuokoa jahazi

October 11th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

WANASOKA Sean Maguire na Daryl Horgan wamejumuishwa katika timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland kwa minajili ya kampeni zijazo za Uefa Nations League dhidi ya Wales na Finland.

Maguire ni mshambuliaji matata wa klabu ya Preston naye Horgan ni fowadi tegemeo kambini mwa Wycombe. Wawili hao wanajaza nafasi za wachezaji Aaron Connolly na Adam Idah katika kikosi hicho cha koch Stephen Kenny.

Connolly na Idah waliondolewa katika kikosi cha Ireland kilichovaana na Slovakia kwenye nusu-fainali ya mchujo wa kufuzu kwa Euro baada ya kubainika kwamba walitangamana kwa karibu sana na afisa wa kikosi aliyeugua Covid-19 kambini.

Connolly, 20, alikuwa apangwe katika kikosi cha kwanza cha Ireland dhidi ya Slovakia mjini Bratislava. Kuondolewa kwake kulipisha kiungo James McClean katika mechi hiyo ambayo Ireland walipoteza 4-2 kupitia penalti baada ya kuambulia sare tasa mwishoni mwa muda wa zaidi ugani Narodny.

Matokeo hayo yalishuhudia Ireland wakipoteza fursa ya kuvaana na Northern Ireland katika mchujo wa mwisho jijini Dublin.

Masogora wa kocha Kenny wamepangiwa kuvaana na Wales uwanjani Aviva mnamo Oktoba 11, 2020 kabla ya kutua Helsinki kupepetana na Finland mnamo Oktoba 14, 2020.