Makala

IRENE NZUKI: Ndoto yangu ya kuwa mwigizaji itatimia

September 24th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika kazi zake na kutambulika kote duniani. Irene Mumbua Nzuki aachwi nyuma ni miongoni mwa kina dada wanaopania kujizolea umaarufu si haba hapa nchini pia kimataifa akilenga kuibuka kati ya wasanii tajika.

Anaamini akipewa nafasi anacho kipaji cha kutesa katika tasnia ya uigizaji na kufaulu kutwaa tuzo ya mwana maigizo bora wa kike kwenye tuzo za Grammy Awards ndani ya miaka mitano ijayo.

Mumbua (21) anadokeza kuwa ingawa hajapata mashiko katika jukwaa la uigizaji anaamini kwamba ipo siku kazi yake itakumbalika kote duniani. ”Bila kujipigia debe nina imani nitafanya vizuri katika maigizo wala sina shaka kabisa ingawa ningali shuleni,” anasema na kuongeza analenga kufikia kiwango cha mwigizaji wa kimataifa, Julia Montes mzawa wa Ufilipino.

MWANAHABARI

Anaamini hivi karibuni atafanya filamu na kupata mpenyo kupeperushwa kwenye runinga. Binti huyu ni mwanafunzi wa mwaka wa pili kwenye Chuo Kikuu cha East Africa Institute of Certified Studies (ICS) anakosomea kuhitimu kwa shahada ya diploma kama mwanahabari wa runinga.

”Katika mpango mzima ingawa ninasomea uanahabari binafsi tangia utotoni mwangu nilitamani sana kuhitimu kuwa mwigizaji wa kimataifa lakini unajua nini kama mwanadamu ni vyema kuwa na mpango mbadala,” akasema na kuongeza kwamba alivutiwa na uigizaji alipoanza kutazama filamu za msanii wa Bongo, Wema Sepetu.

Anasema alipata motisha zaidi akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili kwenye ya Kakuyuni Secondary baada ya kusalitiwa na wenzake shuleni humo.

”Kipindi hicho nilianza kujituma zaidi katika masuala ya maigizo ili kujiepusha na maisha ya upweke. Kando na masomo filamu iligeuka kuwa rafiki wa kulituliza mawazo,” Mwigizaji huyu anayejivunia kushiriki filamu moja iitwayo Morio anasema ameshiriki majiribio mara nyingi tu lakini kupata nafasi imeibuka donda sugu.

Kama wasanii wengine pia angependa kufanya kazi na wenzake ambao wamepiga hatua kisanaa. Anasema anatamani sana kufanya kazi na Brenda Wairimu ambaye ameshiriki filamu kama Mali kati ya zingine. Kwa waigizaji wa Afrika anatamani sana kufanya kazi na Wema Sepetu (Tanzania) na Omotola Jalade(Nigeria) anayejivunia kushiriki filamu kama ‘Tie that Bind,’ ‘Blood Sister,’ ‘A private Storm,’ na ‘Alter Ego,’ kati ya zingine.

Anashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono kwenye juhudi za kupalilia kipaji chake katika ulingo wa burudani na kusema kuwa kwa jumla familia yake humpa motisha zaidi jambo ambalo humfanya aamini ipo siku itakumbalika.