Makala

Ireri alivyokuwa ombaomba na chokoraa, ila sasa yuko Olimpiki ya Walemavu jijini Paris

Na GEOFFREY ANENE August 17th, 2024 2 min read

ALIYEKIUWA ombaomba na chokoraa mitaani Nairobi, Dedan Ireri, amezamia mazoezi mjini Compiegne nchini Ufaransa tayari kwa Michezo ya Olimpiki za Walemavu itakayofanyika mjini Paris mnamo Agosti 28 hadi Septemba 8.

Kenya pia itawakilishwa na muedeshaji mwingine wa baiskeli Kennedy Ogada kwenye michezo hiyo ya haiba.

Ireri na Ogada ni mabingwa wa Afrika mbio za baiskeli za walemavu. Watashiriki mbio hizo ndani ya ukumbi (velodrome) na pia zile za barabarani kwenye michezo hiyo inayofanyika kila baada ya miaka minne. Itakuwa mara yao ya kwanza kabisa kushiriki Olimpiki.

Mwanzoni, Ireri aliandikisha historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza kuzoa medali nne kwenye mashindano ya Afrika (CAC) mnamo Juni 26-27 mjini Cairo, Misri.

Ireri alitawala mashindano ya “time trial” ambayo mshindi ni yule amekamilisha umbali fulani kwa kasi nzuri kuliko wapinzani wake ukumbini (velodrome) na barabarani (C2).

Mwanzoni Ireri alikuwa amepewa tiketi ya kushiriki mbio za barabarani pekee.

Ogada amefuzu kushiriki kitengo cha “tandem” pekee cha B1.

Ogada akishirikiana na Peter Njoki, alifuzu wakati wa Michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Birmingham, Uingereza mwaka 2022 alipokamata nafasi ya sita kwa dakika 1:20.172, huku Neil Fachie (mwelekezi wake Lewis Stewart) wakinyakua taji kwa rekodi ya mashindano hayo sekunde 59.938.

Ogada na mwelekezi Benson Njuguna walishinda dhahabu katika “time trial tandem” barabarani kitengo cha B1 kwa dakika 39:16, lakini wakaridhika na fedha kwa 57:55 baada ya kupoteza dhidi ya Ibrahim Ettesh (Mohamed Emara) kutoka Misri. Matokeo hayo yalitosha kumpa tiketi ya Olimpiki.

Mwendesha baiskeli kitengo cha walemavu Dedan Ireri akipangapanga mabegi anayouza katika barabara za katikati mwa jiji. Yupo kwenye Team Kenya itakayopeperusha bendera ya taifa katika mashindano yatakayoanza Agosti 28, 2024. Picha|Francis Nderitu

Ogada, 52, alipoteza uwezo wa kuona miaka 15 iliyopita, na Ireri, 44, ambaye mguu wake wa kulia ulikatwa akiwa na umri wa miaka tisa baada ya ajali ya barabarani, wamekuwa wakifanya mazoezi katika kaunti ya Murang’a kwa wiki tatu sasa.

“Tumekuwa na mazoezi mazuri nchini Kenya ambako tulikuwa tukikamilisha kilomita 130 kila Jumapili kwa hivyo naweza kusema tuko tayari kabisa kwa Olimpiki na tunalenga dhahabu pekee,” akasema Ogada.

Ireri, ambaye alitoroka shule na kuwa chokoraa, mnyakuzi na mjumbe, sasa ni mchuuzi.

Yuko tayari kuonyeshana ubabe na wakali wa uendeshaji wa baiskeli walemavu.

“Kufuzu kushiriki Olimpiki ni kitu kikubwa kwangu, kinafurahisha na siku kitu cha kawaida,” alisema Ireri. “Nadhani Mungu wakati mwingine hupitisha mtu katika changomoto ili akuandae kwa makubwa na sasa niko katika Olimpiki,” akasema Ireri.

Ireri alitumia fidia alipata baada ya kugongwa na basi na kukatwa mguu kununua baiskeli.

“Nilinunua baiskeli kujifurahisha, lakini baada ya kukutana na mwendeshaji baiskeli mlemavu Ibrahim Wafula, ambaye aliwahi kuwakilisha Kenya kimataifa, kulinibadilisha kabisa mwaka 2004. Alikuwa na mguu mmoja kama mimi,” akasema Ireri.

Ireri alifuzu kushiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza mwaka 2008 baada ya kufanya vyema kwenye mashindano ya dunia mwaka 2007 nchini Colombia, lakini mawasiliano mabovu yakasababisha apoteze fursa hiyo.

Ireri alifichua kuwa mazoezi zaidi kambini kutokana na usaidizi wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Walemavu Kenya na Shirikisho la Uendeshaji Baiskeli Kenya yamemsaidia sana kuimarika.

Mbali na uendeshaji wa baiskeli, Kenya pia itashiriki taekwondo, unyanyuaji uzani, upigaji makasia na riadha kwenye Olimpiki za Walemavu.