Habari Mseto

Isaac Ruto akanusha kutumiwa helikopta na Ikulu

May 13th, 2020 2 min read

Na VITALIS KIMUTAI

KIONGOZI wa Chama Cha Mashinani (CCM), Isaac Ruto, amekanusha madai kwamba Jumatano asubuhi alitumiwa helikopta kumchukua kutoka nyumbani kwake Bomet hadi Ikulu ya Nairobi.

Habari hizo zilidai kwamba alikuwa katika harakati za kuteuliwa waziri.

Madai hayo yalizua joto la kisiasa wakati huu ambao inadaiwa Rais Uhuru Kenyatta anapanga kubadilisha baraza la mawaziri kwa kuteua wataalamu na wanasiasa kutoka vyama tofauti.

Bw Ruto alifafanua kwamba ni kweli alisafiri hadi Nairobi kutoka nyumbani kwake mashambani kijiji cha Tumoi Chepalungu, Kaunti ya Bomet akiwa na mkewe na wakatua uwanja wa ndege wa Wilson na kwamba safari hiyo haikuwa na uhusiano wowote na Ikulu.

“Ni kweli, nilisafiri kwa ndege kutoka Bomet hadi Nairobi nikiwa na mke wangu ambaye hufanya kazi katika sekta muhimu na alihitajika kazini na mwajiri wake jijini Nairobi,” Bw Ruto alisema akiwa uwanja wa ndege wa Wilson.

“Tunapozungumza, ninasubiri gari langu lije kunichukua hadi nyumbani kwangu hapa Nairobi. Ninashangazwa na habari zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusisha safari yangu na miungano ya kisiasa nchini,” aliongeza Bw Ruto.

“Ni kawaida yangu kutumia helikopta kwa sababu inajulikana kwamba nimekuwa nikitumia usafiri wa aina hiyo kwenda maeneo tofauti. Watu hawafai kuhusisha hili na mambo mengine,” alisema.

Bw Ruto ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Magavana amekuwa akishirikiana na mwenyekiti wa chama cha Kanu, seneta wa Baringo Gideon Moi baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 alipokuwa kinara mwenza wa muungano wa Nasa.

Kwenye uchaguzi wa marudio ambao muungano wa Nasa ulisusia, alimuunga Rais Uhuru Kenyatta.

Kumekuwa na tetesi kwamba gavana huyo wa kwanza wa Kaunti ya Bomet na aliyekuwa mbunge wa Kuresoi Kusini Zakayo Cheruiyot wangeteuliwa katika baraza la mawaziri.

Bw Cheruiyot alikuwa katibu wa kudumu katika serikali ya hayati Daniel Moi naye Ruto alikuwa waziri wa masuala ya ufundi na mazingira wakati wa utawala wa Moi.

Isaac Ruto na Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakitofautiana kisiasa mara kwa mara.