Habari MsetoSiasa

Isaac Ruto amkosoa Raila kwa kushirikiana na Uhuru

October 2nd, 2018 1 min read

Na ANITA CHEPKOECH

ALIYEKUWA Gavana wa Bomet, Bw Isaac Ruto, amekosoa mwafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga, akisema una nia ya kufanikisha maazImio ya kibinafsi.

Kiongozi huyo wa Chama Cha Mashinani (CCM) ambaye aliunga mkono ugombeaji wa Bw Odinga katika uchaguzi wa urais mwaka uliopita, katika Muungano wa NASA alikosoa uamuzi wa Bw Odinga kushirikiana na serikali.

Akizungumza katika Shule ya Msingi ya Koitalel iliyo Wadi ya Boito, Kaunti Ndogo ya Konoin, Kaunti ya Bomet, Bw Ruto alisema upande wa upinzani huwa muhimu katika kukuza demokrasia ya nchi ilhali sasa inaonekana upinzani umeangamizwa.

“Raila ndiye angefaa kuhakikisha serikali inatimiza mahitaji ya wananchi, lakini alifanya makosa kwa kuweka mwafaka na Bw Kenyatta. Wanaoumia katika mpango huu wote ni wananchi,” akasema.

Alieleza kuwa kwa kawaida inahitajika serikali iwe inalisha Wakenya na upinzani uchungulie dirishani kuhakikisha chakula kinapikwa na kupakuliwa vyema.

“Kama serikali inakula chakula hicho au kuficha sehemu yake, ni jukumu la kiongozi wa upinzani kufichua hilo na kukomesha ufujaji. Lakini ilivyo kwa sasa, upinzani unaonekana ulipewa sehemu ya chakula kupitia kwa dirisha. Upinzani uliacha kutekeleza majukumu yake,” akasema.

Alikuwa ameandamana na Mbunge wa Konoin, Bw Brighton Yegon, miongoni mwa viongozi wengine katika harambee ya kuchangisha pesa za kushtaki kampuni ya majani chai ya Brooke Bond ambayo ilidaiwa kunyakua ekari 500 za ardhi ya kijamii.

Gavana huyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Magavana, alilaumu ushirikiano huo wa Bw Odinga na serikali kwa kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2018 ambao ulisababisha ongezeko la bei ya mafuta kwa kuweka ushuru wa asilimia nane kwa bidhaa za mafuta.