Na GITONGA MARETE
UVUMI umesambaa kuwa wandani wawili wa aliyekuwa Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi huenda wakapewa nyadhifa za uongozi katika serikali ya Gavana Kawira Mwangaza.
Hilo linatokana na hatua ya Bi Mwangaza kuafikiana nao baada ya jitihada za kumtimua mamlakani kugonga mwamba.Bw Gideon Kimathi na Victor Murithi wiki hii walimaliza tofauti zao na Bi Mwangaza baada ya mzozo baina yake na madiwani wa Meru ambao walipitisha mswada wa kumtimua mamlakani Desemba 14,2022.
Wapinzani hao wameafikiana kufanya kazi na Bi Mwangaza kupitia “handisheki”.
Bunge la Seneti ilitupilia mbali madai 62 yaliyowasilishwa dhidi ya Bi Mwangaza na Diwani wa Abogeta Magharibi, Bw Daniel Kiogora katika mswada uliowasilishwa katika bunge la Kaunti kumwondoa mamlakani gavana huyo.
Naibu Rais Rigathi Gachagua ameitisha mkutano wa kuwapatanisha madiwani wa bunge hilo na Bi Mwangaza.
Kulingana kiongozi wa Wengi, Bw Evans Mawira wa wadi ya Mitunguu alifichua kuwa Bw Gachagua atafanya mkutano huo wa upatanisho katikati ya mwezi huu wa Februari.
Huku kukiwa na nyadhifa kadhaa katika serikali ya Bi Mwangaza huenda gavana huyo akawateua ili awe na udhibiti kamili.
Bunge la kaunti hiyo liliwakataa mawaziri saba kati ya 10 waliopendekezwa na Bi Mwangaza na kupelekea nyadhifa hizo kusalia wazi.
Kwa mujibu wa mdokezi katika kaunti hiyo, kandarasi ya afisa mkuu Rufus Miriti imetamatika na huenda Bw Kariithi kutoka Tigania Magharibi akatwaa wadhifa huo.
Bw Kimathi, aliyekuwa afisa mkuu katika serikali ya Bw Murungi alibwangwa alipowania kiti cha Imenti kusini na Dkt Shadrack Mwiti, naye Bw Kariithi akalambishwa sakafu na Bw Jim Muchui katika kinyang’anyiro cha Wadi ya Athwana katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Wawili hao waliwania nyadhifa hizo kwa tikiti ya chama cha Bw Murungi cha DEP almaarufu “Bus” lakini wakitifuliwa kivumbi kwa kumuunga mkono Bw Raila Odinga wa Azimio la Umoja.
Wakati wa mahojiano na Taifa Leo, wawili hao (Bw Gideon Kimathi na Victor Murithi ) walisema huo ni uamuzi wa “binafsi” kwa kuwa Bw Murungi amestaafu rasmi katika siasa ilhali wao ni wachanga kisiasa na wanahitaji kukomaa.
“Kiraitu amestaafu kisiasa na kwa vile niko na uzoefu katika masuala mbali mbali kwa hivyo nimeamua kuunga mkono serikali kwa lengo la kustawisha kaunti ya Meru,” alisema Bw Kimathi ambaye alikuwa diwani naibu Spika katika bunge la kwanza.
Lakini Bw Kimathi alikataa kukiri ikiwa atajiunga na Serikali ya Bi Mwangaza endapo atapewa fursa.
Kwa upande wa Bw Kariithi alisema “sina shida kufanyakazi na gavana Mwangaza ikiwa hatua hii itafaidi wakazi wa Kaunti ya Meru.”
“Kufuatia kustaafu kisiasa kwa Bw Murungi tuko na jukumu kuunga mkono serikali iliyopo.Sitakuwa na shida kufanyakazi na Bi Mwangaza,” Bw Kariithi alisema wakati mahojiano wakati wa mahojiano.
Akizugumza kwa mara ya kwanza wiki tatu baada ya bunge la Seneti kukataa jaribio la kumtimua Bi Mwangaza, Bw Murungi alisema “kila mtu amekubali kwamba Kawira alishinda.”
Subscribe our newsletter to stay updated