Kimataifa

Israel sasa yaondokea Hospitali ya Shifa ikiwa imeiharibu kabisa

April 2nd, 2024 2 min read

Na MASHIRIKA

JERUSALEM/CAIRO

WANAJESHI wa Israel wameondoka hospitali ya Al Shifa katika mji wa Gaza City baada ya operesheni ya wiki mbili wakiacha vifusi vya majengo yaliyoporomoshwa na miili ya Wapalestina iliyotapakaa kote humo.

Mamia ya wakazi wa Ukanda wa Gaza Jumatatu walifika katika eneo la karibu na hospitali hiyo kubwa zaidi kukagua kiwango cha uharibifu katika mitaa ya karibu baada ya mapigano makali kati ya wanajeshi ya Israel na wapiganaji wa Hamas.

Israel ilisema wanajeshi wake waliwaua na kuwazuilia mamia ya wapiganaji hao kwenye mapigano katika maeneo yanayokaribiana na hospitali hiyo.

Aidha, walinasa idadi kubwa ya silaha na stakabadhi zenye habari za kijasusi.

Msemaji mmoja wa Shirika la Uokoaji wa Dharura katika Gaza alisema wanajeshi wa Israel waliwaua watu wawili zaidi ambao miili yao ilipatikana katika jengo la hospitali hiyo, mikono yao ikiwa imefungwa pingu.

Wafanyakazi wa shirika walitumia mitambo ya buldoza kuchimbua maeneo ya karibu na jengo hilo na kufukua miili mingine.

Wanahabari hawakuthibitisha madai hayo ya mauaji na Idara ya Jeshi ya Israeli haikutoa kauli yoyote kuhusu madai hayo.

Hata hivyo miili ya Wapalestina waliouawa ilionekana katika video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii.

Baadhi miili hiyo iliyofunikwa kwa blanketi chafu ilitapakaa ndani ya jengo hilo la hospitali ambayo kuta zake zilibomoka.

Video hizo zilionyesha sehemu kubwa ya eneo karibu na hospitali ikiwa imechimbuka huku majengo yaliyo karibu yakiwa yamebomolewa au kuteketezwa.

“Nimekuwa nikilia tangu nilipowasili hapa kutokana na mauaji ya halaiki yaliyotekelezwa na wavamizi,” akasema Samir Basel akiongea na wanahabari alipotembelea Al Shifa.

“Sehemu hii imeharibiwa, majengo yameporomoshwa na kuteketezwa. Eneo hili linahitaji kujengwa upya. Hospitali ya Shifa haipo tena,” akaongeza.

Israel ilisema operesheni ndani ya Al Shifa iliendeshwa “huku hatua zikichukuliwa kuzuia madhara kwa raia, wagonjwa na wahudumu wa afya.”

Afisi ya habari ya Ukanda wa Gaza, inayoendeshwa na Hamas, ilisema wanajeshi wa Israel waliwaua Wapalestina 400 katika eneo la Al Shifa.

Miongoni mwa waliouawa ni watoto daktari wa kike na mwanawe ambaye pia ni daktari. Mauaji hayo yalikwamisha shughuli katika hospitali iliyopokea idadi kubwa ya wahasiriwa wa vita.

Israeli haikujibu madai hayo.

Kwa ujumla zaidi ya Wapalestina 32,000 wameuawa wakiwemo wengine 63 ndani ya saa 24 zilizopita, tangu Israel ilipoanza mashambulio katika Gaza mnamo Oktoba 7, 2023. Hizi ni takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya katika eneo hilo.

Wakati huo huo, nchini Misri, wapatanishi walifanya mazungumzo na maafisa wa Israel kwa lengo la kuwashawishi kuelewana na Hamas kuhusu kusitishwa kwa vita.

Lakini afisa mmoja wa Palestina mwenye ufahamu kuhusu juhudi hizo aliwaambia wanahabari kwamba, “hamna dalili ya makubaliano kufikiwa.”