KimataifaMakala

Israel yafanikiwa kuchapisha moyo wa kwanza wenye mishipa kupitia 3D

April 16th, 2019 2 min read

MASHIRIKA na DANIEL OGETTA

MNAMO Jumatatu, wanasayansi wa Israel kwa mara ya kwanza, walifanikiwa kuchapisha moyo wenye tishu na mishipa kwa mfumo wa 3D na kutaja ufanisi huo kama ‘mwamko mpya ambao utawezesha uhamishaji wa viungo vya mwili.’

Japo ni jaribio nzuri baada ya juhudi za awali kufeli, wanasayansi wanaamini kwamba siku moja watakuwa na uwezo wa kuchapisha mioyo yenye uwezo wa kupachikwa kwa binadamu na kuondoa mioyo yenye maradhi.

Mioyo hii iliyochapishwa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Tel Aviv inatoshana na ya sungura kwa ukubwa.

“Ni mara ya kwanza kwa yeyote kufanikiwa kuhandisi na kuchapisha moyo mzima ulio na seli, mishipa ya damu na vijisehemu vyake,” akasema Tal Dvir, msimamizi mkuu wa mradi huo.

“Kwa miaka iliyopita, watu wamefanikiwa kuchapisha michoro ya moyo kwa mfumo wa 3D ila bila seli na mishipa ya kusukuma damu,” aliongeza.

Wanasayansia walieleza kuwepo kwa changamoto nyingi kabla ya kufanikishwa kwa uchapishaji na uhamishaji wa mioyo hiyo kwa wagonjwa.

Jumatatu katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv, wanahabari walionyeshwa uchapisho wa moyo kwa mfumo wa 3D wenye kiasi cha ngarange uliotumbukizwa kwenye kioevu huku watafiti wakitangaza matokeo ya utafiti yaliyokuwa yamechapishwa kwenye kijitabu cha Advance Science.

Watafiti sasa wanapaswa kufunza mioyo iliyochapishwa kuwa na muonekano na utendakazi sawia na mioyo halisi. Seli zingali na uwezo wa kujikunja huku zikikosa uwezo wa kusukuma damu.

Dvir alikadiria kuwa kwa takriban mwaka mmoja hivi, watakuwa wamejipanga vyema na jinsi ya kuihamishia kwa wanyama.

“Pengine, kwa miaka kumi ijayo, kutakuwepo na mashine ya kuchapisha vyombo hivi katika hospitali za ngazi ya juu duniani na taratibu hizi zitafnywa kila mara,” akasema.

Japo alisema kuwa hospitali zitalazimika kuanzia kwa vyombo vyepesi kama nyoyo.

Wakivumbua utafiti huu, Chuo Kikuu cha Tel Aviv kililitaja uvumbuzi huu kama ufunuo mkubwa katika ulingo wa afya.

Wengi wa wagonjwa wa moyo huaga dunia kutokana na idadi ndogo ya wafadhili. Na iwapo wanafaidika, bado wanaweza kuathirika kutokana na miili yao kukataa uhamishaji wa kuingo hicho – changamoto ambayo watafiti wanafanya juu chini kusuluhisha.

Katika harakati ya utafiti wao, walichunguza tishu ya mafuta kutoka kwa mgonjwa, ambayo ilitumika katika kutengeneza wino wa kuchapisha katika mfumo wa 3D.

Kwanza, vijisehemu vya moyo wa mgonjwa vilitengenezwa kisha moyo mzima.

Kutumia tishu ya mgonjwa mwenyewe kulikuwa wa umuhimu wa kuondoa hatari ya uhamiaji wa kiungo hicho kukataliwa na mwili wenyewe, Dvir alieleza.

“Uhandisi wa utangamano wa nyenzo hizo ni muhimu katika kuondoa hatari ya kutatuliwa kwa uhamishaji wa viungo kwani utazuia ufanikishaji wa matibabu hayo,” Dvir akasema

Mojawapo ya changamoto zilizobaki ni jinsi ya kuongeza ukubwa wa seli ili iwe na tishu ya kutosha ya kuutengeneza upya moyo wenye usawa na ule wa binadamu, alisema.

Mashine iliyoko ya kuchapisha katika mfumo wa 3D pia inakumbwa na upungufu wa mwonekano, pamoja na ugumu wa kutambua jinsi ya kuzichapisha mishipa ya damu.

Japo uchapisho huu wa mfumo wa 3D haukuwa wa kisasa na wenye ukubwa wa moyo wa sungura tu, mioyo yenye ukubwa sawa na wa binadamu inaweza kuchapishwa kupitia tecknolojia hii hii.

Teknolojia hii imestawi kuwezesha machapisho ya mifumo ya 3D ya kila kitu hasa katika mapishi, ujenzi na uundaji wa silaha.