Isuzu EA yapangia Kipchoge mapokezi motomoto

Isuzu EA yapangia Kipchoge mapokezi motomoto

Na GEOFFREY ANENE

KAMPUNI ya magari ya Isuzu East Africa imeeleza kufurahia balozi wake wa magari ya D-Max, Eliud Kipchoge aliyehifadhi taji la mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki 2020 nchini Japan mnamo Agosti 8.

Kipchoge,36, alitwaa taji kwa saa 2:08:38 baada ya kuwa mbele pekee yake zikisalia kilomita 10.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya wanaume ya umbali huo ya saa 2:01:39 kutoka ushindi wake wa Berlin Marathon mwaka 2018, amekuwa balozi wa magari ya D-Max tangu mwaka 2017.

“Tunafurahi sana, kuvutiwa na kujivunia na mafanikio ya Kipchoge kwenye Olimpiki na pia kushirikiana naye. Imekuwa safari ndefu na inaendelea kuwa ya kusisimua. Tuna hamu ya kuendelea na ushirikiano huu hata zaidi,” kampuni hiyo imeambia Taifa Leo, Agosti 9, 2021 kupitia kwa afisa wake wa mawasiliano Dancan Muhindi.

Alifichua kuwa kampuni hiyo inapanga kumuandalia mapokezi katika makao yake makuu yanayopatikana katika barabara ya Mombasa Road.

Kufikia mwaka 2020, mfalme huyo wa marathon alikuwa amepokea Sh30 milioni kutoka kwa Isuzu East Africa ikiwemo kupewa gari la D-Max alipovunja rekodi ya dunia ya 2:02:57 iliyowekwa na Mkenya Dennis Kimetto katika Berlin Marathon mwaka 2014 na lingine mwaka 2019 alipoingia katika mabuku ya historia kwa kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili. Alitimka mbio maalum za INEOS1:59 Challenge mwezi Oktoba 2019 kwa saa 1:59:40 jijini Vienna, Austria.

Tangu isaini kandarasi na Kipchoge, kampuni hiyo inasema kuwa soko lake limeimarika kutoka asilimia 19 hadi 29 katika kipindi cha kwanza cha miaka mitatu.

Kwenye Olimpiki 2020, Kipchoge alifuatiwa kwa karibu na Mholanzi Abdi Nageeye (2:09:58) na Mbelgiji Bashir Abdi (2:10:00), huku Mkenya mwingine Lawrence Cherono akikamata nafasi ya nne (2:10:02) naye Amos Kipruto alikuwa katika orodha ya wakimbiaji 30 ambao hawakumaliza. Kipchoge na Wakenya wenzake wanatarajiwa kuondoka Japan kurudi nyumbani mnamo Agosti 9.

Huenda Kipchoge akaelekea nyumbani kwake mjini Eldoret katika kaunti ya Uasin Gishu kwanza kabla ya kurejea jijini Nairobi kwa mapokezi ya Isuzu East Africa.

Nchini Japan, Kenya ilizoa medali ya dhahabu pia kupitia kwa Peres Jepchirchir (marathon ya kinadada), Emmanuel Korir (mita 800) na Faith Chepng’etich (mita 1,500). Hellen Obiri (mita 5,000), Ferguson Rotich (mita 800), Brigid Kosgei (marathon) na Timothy Cheruiyot (mita 1,500) walizoa medali za fedha nao Benjamin Kigen na Hyvin Kiyeng wakaridhika na nishani za shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

You can share this post!

Real Madrid na AC Milan nguvu sawa huku Bale akipoteza...

Tuanzebe ajiunga na Aston Villa kwa mkopo kwa mara ya tatu