Michezo

'Itakuwa unafiki timu zikimwaga mabilioni tena kusaka vipaji'

June 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

AFISA Mkuu Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward, amesema kwamba itakuwa kinaya na dhihirisho la unafiki miongoni mwa wasimamizi wa soka kote duniani iwapo vikosi vya soka vitamwaga sokoni mabilioni ya fedha kwa minajili ya kujisuka upya msimu ujao.

Kwa mujibu wa Ed Woodward, itakuwa busara zaidi kwa waendeshaji wa soka, hasa ya bara Ulaya, kuelekeza fedha walizonazo katika hazina zao katika juhudi za kukabiliana na janga la corona badala ya kujiandaa kujishughulisha katika soko la uhamisho wa wachezaji katika misimu ijayo.

Kinara huyo pia amefichua kuwa huenda sasa wakajiondoa kwenye vita vya kuwania huduma za mvamizi matata wa Tottenham Hotspur, Harry Kane na kiungo chipukizi wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho.

Awali, Man-United walikuwa radhi kuweka mezani kima cha Sh28 bilioni kwa minajili ya Kane na pia kutumia zaidi ya Sh18 bilioni ili kuyapata maarifa ya Sancho ambaye pia anawaniwa pakubwa na Chelsea, PSG, Real Madrid na Bayern Munich.

“Tunatambua ugumu wa hali katika sekta ya michezo kwa sasa. Mambo si kawaida. Itakuwa vyema kwa vikosi, katika viwango vyao, kuingilia kati vita hivi vya kukabiliana na corona,” akatanguliza.

“Haitakuwa picha nzuri kufungulia mifereji ya fedha wakati wa uhamisho na kujinasia huduma za wachezaji wa haiba kubwa mwishoni mwa msimu huu wakati ambapo tunazidi kushuhudia athari mbaya za virusi hivi,” akaongeza.

Ed Woodward anataka vikosi vyote vya soka ya bara Ulaya kushikana mikono na kupiga jeki juhudi za serikali mbalimbali hadi janga la corona litakapodhibitiwa vilivyo badala ya klabu kuchukulia mambo kuwa kawaida na kuanza kujifua kwa mihula ijayo.

Kujiondoa kwa Man-United miongoni mwa klabu ambazo zimekuwa zikimhemea Kane sasa huenda kukawapisha Juventus na Real Madrid ambao pia wamekuwa wakimvizia fowadi huyo mzawa wa Uingereza.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, huenda Tottenham wakawa radhi zaidi kumuuza Kane ili kupunguza gharama ya kumdumisha kimshahara na pia wajipe fedha zitakazowawezesha kujisuka upya.

Ukubwa wa gharama ya kuwadumisha baadhi ya masupastaa wao, ni kati ya sababu zilizowachochea Tottenham pia kuagana na kiungo matata mzawa wa Denmark, Christian Eriksen aliyejiunga na Inter Milan ya Italia mwanzoni mwa mwaka huu.

Katika juhudi za kulijaza pengo la Kane na Eriksen, Tottenham wamefichua azma ya kumsajili kiungo Geoffrey Kondogbia, 27, kwa kima cha Sh9.8 bilioni.

Hii ni baada ya nyota huyo mzawa wa Ufaransa kusisitiza kwamba atakuwa radhi kuagana na Valencia iwapo kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) hakitafanikiwa kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Hata hivyo, itawalazimu Tottenham kuwapiga kumbo Everton ambao pia wanakeshea maarifa ya Kondogbia. Hadi alipotua Valencia, sogora huyo alikuwa pia amewachezea Lens, Sevilla, AS Monaco na Inter Milan.

Iwapo Tottenham wataambulia pakavu katika juhudi za kuwania huduma za Kondogbia, kocha Jose Mourinho amedokeza uwezekano wa kuifukuzia saini ya kiungo wa Barcelona Philippe Coutinho ambaye kwa sasa anachezea Bayern Munich ya Ujerumani kwa mkopo.

Chelsea pia wanayakeshea maarifa ya Coutinho ambaye Bayern watakuwa radhi kabisa kumwachilia iwapo watafaulu kumpata Roberto Firmino wa Liverpool pamoja na kiungo wa Manchester City, Leroy Sane.