Italia kukutana na Uhispania kwenye nusu-fainali za Euro baada ya kuipiga Ubelgiji 2-1

Italia kukutana na Uhispania kwenye nusu-fainali za Euro baada ya kuipiga Ubelgiji 2-1

Na MASHIRIKA

ITALIA waliwakomoa Ubelgiji 2-1 mnamo Ijumaa usiku jijini Munich, Ujerumani na kufuzu kwa nusu-fainali ya Euro itakayowakutanisha na Uhispania mnamo Julai 6, 2021.

Ingawa mchuano huo haukushuhudia idadi kubwa ya mabao yakifumwa wavuni, kila upande ulijituma vilivyo na mashambulizi yakatamalaki mchezo hadi mwisho.

Italia wanaopigiwa upatu wa kutwaa taji la Euro, walijibwaga uwanjani wakipania kuendeleza ubabe wao huku Ubelgiji wakiwa pia na azma ya kusadikisha mashabiki kwamba wanastahili kuorodheshwa katika nafasi ya kwanza kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Ushindi wa Italia ulikuwa wao wa 13 mfululizo huku wakiwa sasa wamesakata jumla ya mechi 32 bila kupoteza.

Chini ya kocha Roberto Mancini, Italia walifungua ukurasa wa mabao kupitia Nicolo Barella aliyeshirikiana na Marco Verratti katika dakika ya 31 kabla ya Lorenzo Insigne kufuma wavuni goli la pili dakika 13 baadaye.

Ubelgiji walirejea mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya Romelu Lukaku kufunga penalti iliyochangiwa na hatua ya Jeremy Doku kuchezewa visivyo na Giovanni de Lorenzo katika dakika ya 45.

Kila kikosi kilipoteza nafasi maridhawa za kufunga mabao katika kipindi cha pili kilichotamalakiwa na shambulizi baada ya jingine.

Pigo la pekee kwa Italia ni kwamba watavaana sasa na Uhispania kwenye nusu-fainali uwanjani Wembley, Uingereza bila ya kujivunia huduma za beki wa kushoto Leonardo Spinazzola aliyepata jeraha la kifundo cha mguu katika kipindi cha pili.

Italia walikamilisha kampeni za Kundi A bila ya kupoteza mechi yoyote katika uwanja wao wa nyumbani wa Olimpico, Roma. Waliwapepeta Uturuki 3-0, wakachapa Uswisi 3-0 na kupokeza Wales kichapo cha 1-0. Ufanisi huo uliwakatia tiketi ya hatua ya 16-bora iliyowashuhudia wakipepeta Austria 2-1 katika muda wa ziada uwanjani Wembley.

Hata hivyo, matokeo dhidi ya Ubelgiji nchini Ujerumani huenda ndiyo bora na muhimu zaidi kwa Italia kuwahi kushuhudia katika kipindi cha takriban miaka mitatu bila ya kushindwa.

Italia walianza mechi kwa matao ya juu huku bao la Leonardo Bonucci katika dakika ya 23 likikataliwa na refa baada ya teknolojia ya VAR kubaini kwamba alicheka na nyavu akiwa ameotea.

Kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia naye alijitahidi vilivyo na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na wavamizi wa Ubelgiji.

Licha ya kuwa kikosi bora kwa sasa duniani, Ubelgiji ambao pia wanajivunia idadi kubwa ya wanasoka wa haiba kubwa, walikamilisha kampeni za Kombe la Dunia katika nafasi ya tatu mnamo 2018 nchini Urusi. Fainali ya mwisho ya Euro ambayo kikosi hicho kimewahi kunogesha ni ya 1980 ambapo walizidiwa ujanja na iliyokuwa Ujerumani Magharibi.

Mabeki wote watatu wa Ubelgiji walikuwa na umri wastani wa miaka 33 huku wanasoka wawili pekee katika kikosi chao cha kwanza cha 11-bora wakiwa na umri wa chini ya miaka 28.

Mbali na Doku, wanasoka wengine wa Ubelgiji ambao walitatiza pakubwa mabeki wa Italia ni Kevin de Bruyne na Lukaku ambaye sasa amefungia kikosi hicho jumla ya mabao 24 kutokana na mechi 23 zilizopita.

Ingawa imesalia miezi 18 pekee kabla ya fainali zijazo za Kombe la Dunia kuandaliwa nchini Qatar mnamo 2022, kinachosubiriwa ni iwapo Ubelgiji bado watakuwa chini ya mkufunzi wao wa sasa, Roberto Martinez.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kaunti pwani zapigwa darubini kuhusu miradi hewa

BBI: Karua adai Uhuru alinyakua mamlaka ya raia