Italia wakomoa Hungary jijini Budapest katika Uefa Nations League

Italia wakomoa Hungary jijini Budapest katika Uefa Nations League

Na MASHIRIKA

ITALIA walifuzu kwa nusu-fainali za Uefa Nations League baada ya kukomoa Hungary 2-0 katika pambano la mwisho la Kundi A3 mnamo Jumatatu usiku jijini Budapest.

Hungary wanaonolewa na kocha Marco Rossi walijibwaga ugani wakihitaji sare ya aina yoyote ugani Puskas Arena ili kutinga hatua ya nne-bora ya kipute hicho kitakachoendelea Juni 2023.

Giacomo Raspadori aliweka Italia kifua mbele katika dakika ya 27 kabla ya Federico Dimarco kukamilisha krosi ya Bryan Cristante kunako dakika ya 52 na kuhakikishia mabingwa hao wa Euro 2020 ushindi.

Matokeo hayo yalikweza Italia kileleni mwa Kundi A3 kwa alama 11 kutokana na mechi sita. Hungary waliodenguliwa kileleni walishuka hadi nafasi ya pili kwa pointi 10, tatu zaidi kuliko Ujerumani ambao waliambulia sare ya 3-3 dhidi ya Uingereza walioteremshwa ngazi baada ya kujizolea pointi tatu pekee.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Italia kushinda jijini Budapest tangu 1996. Kikosi hicho cha kocha Roberto Mancini kilitegemea pakubwa maarifa ya Gianluigi Donnarumma – kipa mzoefu wa Paris Saint-Germain (PSG) aliyepangua makombora mazito ya Hungary.

Italia waliokosa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar, sasa wanaungana na Croatia na Uholanzi kwenye fainali za Nations League mnamo Juni 14-18, 2023. Uhispania na Ureno watapigania nafasi ya mwisho ya kunogesha nusu-fainali usiku wa Septemba 27, 2022 jijini Braga.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uingereza na Ujerumani waambulia sare ya 3-3 katika Nations...

Ufaransa waponea kushushwa ngazi kwenye Uefa Nations League...

T L