Italia wakomoa Uingereza na kutwaa ubingwa wa Uefa Euro 2020

Italia wakomoa Uingereza na kutwaa ubingwa wa Uefa Euro 2020

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Uingereza kutwaa taji la Euro kwa mara ya kwanza na la pili kwenye kipute cha haiba kubwa tangu washinde Kombe la Dunia mnamo 1966, yalizamishwa na Italia mnamo Jumapili usiku katika uwanja wa Wembley jijini London.

Hii ni baada ya Italia kuwapokeza kichapo cha 3-2 kupitia penalti. Mshindi wa gozi hilo aliamuliwa kupitia matuta baada ya pande zote mbili kuambulia sare ya 1-1 kufikia mwisho wa muda wa ziada.

Wakipania kuzoa taji la Euro mwaka huu, Uingereza waliwekwa kifua mbele na beki Luke Shaw aliyetikisa nyavu za Italia baada ya dakika mbili pekee za kipindi cha kwanza.

Japo bao hilo la haraka liliyumbisha uthabiti wa Italia, masogora hao wa kocha Roberto Martinez walidhihirisha kiu ya kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 34.

Walirejea mchezoni katika dakika ya 67 baada ya kufungiwa bao na beki Leonardo Bonucci aliyemzidi maarifa kipa Jordan Pickford baada ya kombora lililovurumishwa na Marco Verratti kugonga mlingoti wa lango la Uingereza.

Uingereza walipoteza penalti tatu. Fowadi wa Manchester United, Marcus Rashford alishuhudia mkwaju wake ukibusu mhimili wa goli kabla ya kipa Gianluigi Donnarumma kupangua penalti za Jadon Sancho na Bukayo Saka walioletwa uwanjani katika dakika za mwisho za mchezo kwa kibarua hicho cha kuchanja matuta.

Harry Kane na Harry Maguire walifunga mikwaju yao huku Pickford akipangua mikwaju ya Andrea Belotti na Jorginho. Wanasoka wa Italia waliofunga penalti zao ni Domenico Berardi, Bonucci na Federico Bernardeschi.

Kabla ya kutinga fainali ya Euro mwaka huu, mara ya mwisho kwa Uingereza kunusia ubingwa wa pambano la haiba kubwa katika ulingo wa soka ni mwaka wa 2018 ambapo walidenguliwa na Croatia kwenye nusu-fainali za Kombe la Dunia jijini Moscow, Urusi.

Mbali na Saka na Sancho, chipukizi wengine ambao sasa wanapigiwa upatu wa kuwa tegemeo la Uingereza kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar ni Phil Foden, Mason Mount, Jude Bellingham na Jack Grealish.

Kwa mujibu wa Mancini, kikubwa zaidi kilichozolea Italia taji la Euro ni mseto mzuri wa chipukizi na wanasoka wa haiba kubwa wanaojivuniwa na kikosi hicho. Aidha, alikiri kwamba masogora wake wamekuwa na kiu ya kudhihirisha ubabe wao kwenye ulingo wa soka tangu wakose kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2018.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia atawazwa Mchezaji Bora...

UDA yapigwa rafu Kiambaa