Italia wakung’uta Uswisi na kuingia hatua ya 16-bora kwenye Euro

Italia wakung’uta Uswisi na kuingia hatua ya 16-bora kwenye Euro

Na MASHIRIKA

ITALIA iliwakung’uta Uswisi katika mechi ya Kundi A kwenye fainali za Euro mnamo Jumatano usiku na kuwa kikosi cha kwanza kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya kipute hicho kilichoahirishwa mwaka wa 2020 kwa sababu ya corona.

Chini ya kocha Roberto Mancini, Italia walifungua kampeni zao za Kundi A kwa kusajili ushindi mwingine wa 3-0 dhidi ya Uturuki mnamo Juni 11 jijini Roma.

Wakicheza dhidi ya Uswisi, kiungo matata wa Sassuolo, Manuel Locatelli, alifungia Italia mabao mawili katika dakika za 26 na 52 baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo Domenico Berardi.

Italia walitamalaki mchezo kuanzia mwanzo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira. Bao lao la tatu lilipachikwa wavuni na fowadi Ciro Immobile aliyemwacha hoi kipa Yann Sommer mwishoni mwa kipindi cha pili.

Wavamizi wa Uswisi hawakutatiza Italia ambao kwa sasa wamepiga jumla ya mechi 10 mfululizo katika mashindano mbalimbali bila kufungwa bao.

Mbali na mabingwa wa dunia Ufaransa na Ubelgiji wanaoshikilia nafasi ya kwanza kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya orodha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kikosi kingine ambacho kwa sasa kinapigiwa upatu wa kutwaa taji la Euro mwaka huu ni Italia.

Italia kwa sasa wanashikilia rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 29 zilizopita. Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kivumbi cha Euro kupulizwa, Italia hawakuwa wamewahi kufunga mabao matatu katika mechi moja.

Pigo la pekee kwa Italia ni jeraha ambalo nahodha Giorgio Chiellini alipata mwishoni mwa kipindi cha pili wakati wa mechi dhidi ya Uswisi.

Jaribio la pekee ambalo Uswisi walifanya langoni pa Italia ni kombora la mwisho wa kipindi cha pili kupitia kwa Steven Zuber aliyemtatiza kipa Gianluigi Donnarumma.

Iwapo Italia watasajili sare au kushinda Wales katika mchuano wa mwisho wa Kundi A mnamo Juni 20, basi watakamilisha kampeni za kundi lao kileleni na kujikatia tiketi ya kuvaana na kikosi kitakachoibuka nambari mbili kwenye Kundi C mnamo Juni 26 uwanjani Wembley.

Kundi C linawajumuisha Austria na Uholanzi wanaojivunia alama tatu kila mmoja, pamoja na Ukraine na Macedonia Kaskazini ambao walipoteza mechi za ufunguzi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Man-City kuanza kutetea ubingwa wa EPL kwa kibarua kizito...

Kizaazaa kortini baada ya kasisi aliyetisha mpenziwe...