Italia watoka sare na Uswisi na kufikia rekodi ya Brazil ya kutoshindwa katika mechi 36 mfululizo

Italia watoka sare na Uswisi na kufikia rekodi ya Brazil ya kutoshindwa katika mechi 36 mfululizo

Na MASHIRIKA

TIMU ya taifa ya Italia ilifikia rekodi ya Brazil ya kutoshindwa katika mechi 36 mfululizo za kimataifa baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Uswisi mnamo Jumapili katika mchuano wa Kundi C wa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Italia ambao ni washikilizi wa taji la Euro 2020, walipoteza nafasi nyingi za wazi huku kiungo matata wa Chelsea, Jorginho, akipoteza penalti katika kipindi cha pili.

Hata hivyo, masogora hao wa kocha Roberto Martinez wangali kileleni mwa Kundi C kwa alama 11, nne zaidi kuliko Uswisi ambao wana mechi mbili zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na Italia.

Sare dhidi ya Uswisi iliwezesha Italia kuvunja rekodi ya Uhispania ambao hawakushindwa katika jumla ya mechi 35 mfululizo kati ya 2007 na 2009. Kwa upande wao, Brazil walipiga jumla ya mechi 36 mfululizo bila ya kupoteza hata moja kati ya 1993 na 1996.

Penalti ya Jorginho ilikuwa fursa maridhawa zaidi kwa Italia almaarufu ‘Azzurri’ kuzamisha chombo cha Uswisi na kurejea katika hali yao ya kushinda mechi baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 na Bulgaria mnamo Septemba 2, 2021 jijini Roma.

Mkwaju huo wa Jorginho ulipanguliwa na kipa Yann Sommer. Ni penalti iliyotokana na tukio la fowadi Domenico Berardi kuchezewa visivyo na Ricardo Rodriguez katika dakika ya 53.

Fowadi wa Italia Domenico Berardi. Picha/ AFP

Mchuano ujao wa Italia ni mnamo Septemba 8, 2021 dhidi ya Lithuania watakaokuwa wakisaka ushindi wao wa kwanza kundini. Uswisi kwa upande wao watakuwa wakipepetana na Ireland ya Kaskazini ugenini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ujerumani wakomoa Armenia 6-0 na kutua kileleni mwa Kundi J...

UN yalaani mapinduzi Guinea