Kimataifa

Italia yaahidi ushirikiano mzuri, yakataza Afrika tabia ya ukupe

January 29th, 2024 2 min read

NA HASSAN WANZALA

BARA la Afrika litatengewa nafasi na kupewa zingatio maalum katika ajenda ya Italia kwenye kipindi chake cha urais wa kupokezana katika muungano wa Mataifa Yaliyostawi Duniani (G7).

Mbali na Italia, G7 inazileta pamoja Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan, Uingereza, na Marekani.

Waziri Mkuu wa Italia Giogia Meloni alitangaza Jumatatu katika Makala ya 25 ya Kongamano Kuu la Italia-Afrika lililoandaliwa jijini Rome kwamba lengo la Italia–iliyochukua urais wa G7 mapema Januari–ni “kubuni sera madhubuti ya ushirikiano wa kimataifa yenye lengo la kuifanya Afrika miongoni mwa ajenda zake katika urais wake G7”.

Meloni alisema hayo alipohutubia viongozi 25 kutoka Afrika na wawakilishi wa taasisi kadhaa za Muungano wa Ulaya waliohudhuria kikao cha kongamano hilo kuu.

“Italia inatambua umuhimu wa ushirikiano na mshikamano baina ya mabara, hivyo tunapaswa kutafakari jinsi tunavyoweza kuufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wetu, kama washirika wenye nguvu zinazotoshana bila hila za ufyonzaji au utegemezi,” akasema Meloni.

Meloni alisema Mpango wa Italia uliopewa jina ‘Mkakati wa Mattei’, unalenga kujenga ushirikiano na Afrika kwa njia inayosaidia kutatua changamoto ya uhamiaji wa kiharamu na pia kugeuza Italia kitovu cha usambazaji wa kawi kutoka Afrika hadi Ulaya wakati ambapo bara hilo linajaribu kadri ya uwezo wake kuepuka utegemezi wa mafuta na gesi kutoka Urusi.

Mataifa mengi ya Ulaya yaliiwekea Urusi vikwazo tangu iivamie Ukraine mnamo Februari 24, 2022.

Mkakati wa Mattei umetengewa bajeti ya Euro 5.5 bilioni (sawa na Sh969 bilioni) ambazo ndani kuna “mikopo, ruzuku, na dhamana”.

Kwa kiwango hicho, Meloni alisema “takriban Euro 3 bilioni zitatoka kwa hazina ya mazingira ya Italia na 2.5 bilioni zitoke kwa mfuko wa ushirikiano wa kimaendeleo”.

Tayari waziri mkuu huyo kwenye mahojiano na kituo cha habari cha TG1 mnamo Jumapili, alifichua mradi wa majaribio wa kituo cha kozi anuwai kuhusu nishati jadidifu umeanzishwa nchini Morocco. Pia alisema miradi mingine ni ya elimu nchini Tunisia, na ile ya kupanua wigo wa huduma za afya nchini Cote d’Ivoire.

Tunisia na Cote d’Ivoire zinashikilia nambari ya pili na ya tatu mtawalia kwa raia wake waliowasili nchini Italia wakiwa ama wahamiaji au wakimbizi kupitia bahari ya Mediterranean mwaka 2023.

Mkakati wa Mattei unatokana na mtumishi wa umma Enrico Mattei, ambaye katika miaka ya hamsini (1950s) alipemdekeza Italia kuunga mkono juhudi za mataifa ya Kaskazini mwa Afrika kukuza chumi zao na kunufaika kutokana na rasilimali zao.

“Mkakati wa Mattei unajikita zaidi katika kugawana rasilimali na ujuzi na hivyo dhamira kuu ya kongamano hili ni kupanga namna ufanisi utakavyopatikana,” akaahidi Meloni.

Alisema miradi mingine itaanza kutekelezwa nchini Kenya, Algeria, Msumbiji, Misri na Jamhuri ya Congo.

Mnamo Jumapili Rais wa Kenya William Ruto alisema lengo kuu la kongamano kuu la Italia-Afrika ni kuunda mtandao wa ushirikiano wa kimaendeleo.

“Kongamano hili linatoa fursa nzuri ya kuunda mikakati ya ushirikiano kuangazia masuala muhimu ya utoshelevu wa chakula, kozi anuwai, kawi na ujenzi wa miundomsingi,” akasema Rais Ruto kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter) mara baada ya kuwasili jijini Rome.

Pembezoni mwa kongamano kuu hilo, Rais Ruto alikutana pia na Mkurugenzi Msimazi wa Ngazi ya Juu katika Benki ya Dunia Axel van Trotsenburg, ambaye anatekeleza wajibu wa Sera ya Maendeleo na Ushirikiano.

“Tumejadili masuala mengi likiwemo Kongamano Kuu lijalo la Muungano wa Kimataifa kuhusu Maendeleo almaarufu IDA21 ambalo Kenya itakuwa mwenyeji,” akasema.

[email protected]